Tuesday, November 17, 2015

MBINGA YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA VIFAA TIBA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kwamba, upatikanaji hafifu wa vifaa tiba, vitenganishi na upungufu wa watumishi wenye taaluma katika kitengo cha huduma za afya ya uzazi na mtoto wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kunaathiri utoaji wa huduma husika kwa wagonjwa.

Vilevile uhaba na ubovu wa magari, katika vituo vya afya kwa ajili ya kubebea wagonjwa ili kuwezesha rufaa ya wazazi na watoto, nalo limekuwa tatizo sugu na changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo ya afya wilayani humo.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya utekelezaji ya huduma za afya ya uzazi na mtoto wilayani Mbinga, kwa mwaka 2015 ambapo wilaya ina jumla ya vituo 63 vya huduma.


Mary Ngonyani ambaye ni Mratibu wa huduma hizo, katika taarifa yake alisema pia mwitikio wa akina mama kuwahi kliniki bado upo chini na hilo linatokana na hisia binafsi za akina mama,  licha ya kuendelea kuhamasisha na elimu kutolewa mara kwa mara.

Kadhalika alisema kuwa akina mama wajawazito 1,982 walijitokeza na kupima Kaswende,  ambapo kati yao 64 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo sawa na asilimia 3.2 ya waliopima.

“Wajawazito 5,852 walipimwa virusi vya ukimwi sawa na asilimia 77.7 ya ufikiwaji wa mahudhurio manne, kati yao 146 sawa na asilimia 2.4 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo”, alisema.

Ngonyani alibainisha kuwa mimba zenye umri mdogo, zimekuwa zikiongoza wilayani humo kwa asilimia 50.3 na akina mama wenye vidokezo vya hatari waligundulika kuwa navyo, ikiwa ni sawa na asilimia 49.9 ya waliohudhuria vipimo vya kitabibu.

Huduma ya uzazi wa mpango inatolewa kwenye vituo 54 vya huduma, ikiwa ni asilimia 78.2 ambapo uhamasishaji na utoaji wa huduma za uzazi unafanyika kupitia wataalamu waliopo katika vituo hivyo na hospitali ya wilaya, na kwamba katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu huduma hiyo ilitolewa kwa akina mama 17,189 sawa na asilimia 56.2 ya walengwa.

Hata hivyo Mratibu huyo alieleza kuwa huduma za afya ya mtoto zimekuwa zikitolewa, jumla ya watoto 5,966 wamepata huduma ya chanjo katika kipindi hicho ambapo watoto 184 kati ya hao walizaliwa na akina mama wenye virusi vya ukimwi, watoto 179 walichukuliwa damu kwa uchunguzi zaidi ya ugonjwa huo na kwamba kati yao watoto sita  waligundulika kuwa nao ambapo mmoja alifariki dunia na waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu katika kitengo cha ushauri nasaha (CTC).

No comments: