Sunday, November 22, 2015

HALMASHAURI MBINGA YAFANYA VIZURI ELIMU YA MSINGI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imefanikiwa kuvuka lengo katika upimaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa asilimia 19.23 katika kipindi cha mwaka huu kwa ufaulu wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya   kidato cha kwanza, mwaka wa masomo 2015/2016.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Hayo yamebainishwa na Ofisa elimu ya msingi wa wilaya ya Mbinga, Samweli Komba kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Venance Mwamengo ambapo ufaulu huo umeongezeka kutoka aslimia 57 ya mwaka 2014  hadi kufikia asilimia 76 mwaka huu. 

Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa mikakati thabiti iliyowekwa na idara ya elimu ya msingi wilayani humo, kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi  asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia darasa la kwanza hadi la darasa la saba jambo ambalo mpaka sasa limefanikiwa katika utekelezaji wake. 

Komba alisema mwaka 2014, shule zilizofanya mtihani wa  Taifa kumaliza darasa la saba zilikuwa 217 ambapo jumla ya wanafunzi 7,561 walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,303  sawa na asilimia 56.92 walibahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari. 


Kutokana na matokeo hayo, idara ya elimu  kwa kushirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga na wadu wengine iliendelea kuboresha kwa kuwa na mitihani  minne ya majaribio ambapo ufaulu wake, ulikuwa mtihani wa kwanza asilimia 33, wa pili asilimia 72, wa tatu 74 na wanne asilimia  80 hali iliyosababisha kuwa na picha ya matokeo mazuri kwa mtihani huo wa darasa la saba kitaifa kuwa mzuri. 

Kwa mujibu wa Komba alifafanua kuwa, matokeo ya mwaka huu 2015 Halmashauri imekuwa ya kwanza kimkoa, ambapo wanafunzi walioandikishwa walikuwa 6,003 waliofanya mtihani walikuwa 5,887 na wasiofanya ni wanafunzi 114 ambapo kati ya idadi hiyo, waliofanya mtihani zaidi ya watoto 5,000 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari. 

Hata hivyo, licha ya mafaniko makubwa waliyoyapata bado wanakabiliwa na changamoto kubwa, ya uwepo wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kila mwaka, kutokana na sababu mbalimbali. 

Komba ametaja changamoto  zilizopo ikiwemo ya utoro, ugonjwa, vifo, uhaba wa miundombinu kama vile nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na kwamba jamii inahamasishwa kuchangia ili kupata miundombinu inayokidhi idadi ya watoto shuleni, hata hivyo mwitikio umekuwa mdogo kwa jamii kushiriki katika shughuli za kujitolea. 

Alisema baadhi ya wazazi wilayani humo, wamekuwa wakiwatumia watoto kwenye shughuli za kiuchumi, kama vile mashambani kwa lengo la kujiongezea kipato, hata hivyo wanaendelea kutoa elimu na kukemea juu ya madhara ya kuwatumikisha watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi za nyumbani.

No comments: