Tuesday, November 17, 2015

MKUU WA WILAYA MBINGA ALIA NA WATENDAJI WAKE

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga.


Na Muhidin Amri,
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imewaagiza watendaji wake wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuandaa mkakati madhubuti wa kuongeza vyanzo vya mapato, vitakavyowezesha halmashauri hiyo kupata fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa akizungumza  na mwandishi wetu ofisini kwake mjini hapa.

Ngaga alisema, Halmashauri ya Mbinga kwa kiasi kikubwa bado inaendelea kutegemea ruzuku kutoka serikali kuu kutokana na kukosa vyanzo vikubwa vya mapato na hata vilivyokuwepo, kumekuwa na udhaifu mkubwa wa usimamizi jambo ambalo linalotoa nafasi kwa wajanja wachache kutumia nafasi hiyo kujinufaisha.


Alisema kuwa kutokana na  udhaifu huo, halmashauri haiwezi kujiendesha katika mambo yake yenyewe na hivyo itaendelea kutegemea  serikali au wafadhili, jambo  ambalo ni hatari kwa sababu pindi serikali itakapowataka kujitegemea kwa kila jambo, itakuwa vigumu kulipa hata mishahara ya watumishi wake.

Kwa mujibu wa  Ngaga, alifafanua kuwa hali hiyo inatokana na uwezo mdogo wa watendaji pamoja na madiwani kuwa na uwezo mdogo wa kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato, ambapo matokeo yake huendelea kutegemea vya zamani ambavyo wanashindwa kuvisimamia vizuri ili waweze kupata mapato makubwa yatakayosaidia kuendesha shughuli zao za kila siku.

“Baadhi ya watendaji tulionao hawapo makini katika kutekeleza majukumu yao, licha ya wilaya kubarikiwa katika uzalishaji wa mazao ya kila aina, lakini bado tupo nyuma ukizingatia kwamba uzalishaji wa mazao ni mkubwa”, alisema Ngaga.

Aliongeza kuwa, kupitia malengo waliyonayo amewataka kuwa makini hasa katika eneo la kuongeza mapato kupitia vyanzo vilivyopo  ambapo kama vitasimamiwa vizuri vitaleta manufaa  kwa halmashuri na kupiga hatua ya kimaendeleo kama ilivyokuwa kwa halmashauri nyingine hapa nchini.

Kadhalika alibainisha kwamba ni ukweli usio na mashaka kuwa Mbinga, ni kati ya wilaya zilizobahatika kuwa na raslimali nyingi ambazo kama watendaji wake na wananchi kwa ujumla, watazifanyia kazi ipasavyo halmashauri itaweza kupiga hatua mbele zaidi.

No comments: