Friday, November 20, 2015

WAANDISHI WA HABARI RUVUMA WAASWA

Na Muhidin Amri,
Songea.

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Robert Mageni amewataka Waandishi wa habari katika mkoa huo, kusaidia kutangaza na kuandika fursa mbalimbali zilizopo katika halmashauri hiyo hatua ambayo itasaidia kuvutia watu wengi, kwenda kuwekeza katika jimbo la Madaba.

Mbali na wito huo, Mageni amewahimiza  kuandika habari nzuri zinazohamasisha wananchi kujikita katika shughuli za maendeleo hususani kwa zile zinazofanywa na wakazi wa jimbo hilo, badala ya kuandika au kutangaza habari za migogoro kwani zinaweza kuhatarisha  kuharibu mahusiano yaliyopo kati ya wananchi na serikali yao.

Mageni alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake katika kijiji cha Madaba, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mahanje  ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephano Mahundi, aliibuka mshindi dhidi ya mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hans Mlelwa.


Mageni ameungana na wadau wengi  katika mkoa wa Ruvuma, kupongeza mchango mkubwa unaofanywa na waandishi wa habari hapa Ruvuma, kuandika habari sahihi na zinazohamasisha wananchi kushiriki katika  shughuli za kimaendeleo.

Alisema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi hapa nchini, lakini iwapo vitatumika vibaya vinaweza kuleta matatizo makubwa kama vile kuibuka kwa mifarakano kati ya wananchi na serikali yao.

Pia alieleza kuwa amewataka wakazi wa jimbo hilo kuangalia namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo, ili  kujiletea maendeleo yao badala ya kukaa na kusubiri kuona watu kutoka nje wakinufaika na rasilimali hizo, jambo ambalo halipendezi.


Mageni amewahimiza pia, wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuahidi kuwa serikali itajitahidi kuwa karibu nao katika suala la pembejeo za kilimo na kutoa ushauri wa kilimo cha kisasa, ili kiwe na tija kwao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: