Wednesday, November 4, 2015

UWT MBINGA YALALAMIKIA WANACHAMA WAKE

Baadhi ya akinamama wa UWT Mbinga mkoani Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja na mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya hiyo, Dokta Robert Elisha walipotembelea hospitalini hapo kuona wagonjwa hivi karibuni.


Na Muhidin  Amri,
Mbinga.
 
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Chama cha Mapinduzi (UWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema, haitawavumilia wanachama wa umoja huo ambao walikisaliti chama katika uchaguzi mkuu  uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, ambapo kinaweka mikakati ya kuwachukulia hatua wale wote walioonekana kwenda kinyume na matakwa husika, ikiwa ni lengo la kulinda heshima na maadili ya chama hicho.

Pendo Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa umoja huo wilayani humo, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanachama wake katika mkutano wao, uliofanyika ukumbi wa jumba la maendeleo mjini hapa.

Alisema baadhi ya wanachama, walishindwa kukisaidia chama katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu huku wengine wakipigia debe vyama vya upinzani, ili CCM kisiweze kupata ushindi katika uchaguzi huo.


Ndumbaro alisema kuwa wanachama vigeugeu, mara nyingi ndiyo wanaoanzisha mizengwe na vurugu za hapa na pale ndani ya chama hali ambayo inakiweka chama katika wakati mgumu, na kutoa nafasi kwa vyama vya vingine kuendelea kujiimarisha hata kama havina  idadi  kubwa ya wanachama.

Kwa mujibu wa Ndumbaro alidai kwamba wanachama wa aina hiyo ni hatari ndani ya chama kwa kuwa wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi na sio chama, hivyo muda umefika kuwachukulia hatua ili kuepukana na kundi kubwa la wanachama ambao ni mamluki wanaoweza kuleta mifarakano isiyokuwa ya lazima.

Alibainisha kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, UWT imejipanga vizuri na kuhakikisha wale wote watakaoteuliwa kugombea nafasi za uongozi ndani ya umoja huo, ni watu wanaokubalika ndani ya chama na kwa wananchi ili kuepusha chama kufanya vibaya kama ilivyotokea kwa baadhi ya maeneo hapa nchini.

Hata hivyo alisema wameshaanza kuwafuatilia kimya kimya, baadhi ya wanachama wake na iwapo watabainika kukiuka taratibu husika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

No comments: