Thursday, November 5, 2015

MBINGA WANUNUA MTAMBO WA KUNYONYA MAJI TAKA

Gari ambalo limenunuliwa kwa ajili ya kunyonya maji taka, mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imeweza kuondokana na mfumo wa kukodi gari la kunyonya maji taka kutoka Manispaa ya Songea mkoani humo, baada ya kununua gari lake ikiwa ni mikakati yake ya kuhakikisha kwamba wakazi wa mji huo wanaondokana na kero hiyo.

Gari hilo ambalo ni aina ya FAW lenye namba za usajili, SM 11483 limenunuliwa kwa fedha za kitanzania, shilingi milioni 164,654,000.

Akizungumza na mwandishi wetu, Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya mji wa Mbinga, Oscar Yapesa alisema kuwa lengo la kununua gari hilo ni mpango uliowekwa muda mrefu, ili kuweza kuboresha makazi na mazingira ya mji huo kuwa katika hali nzuri.


Yapesa aliongeza kuwa, awali halmashauri hiyo ilikuwa ikitumia gharama kubwa kukodi gari la kunyonya maji taka kutoka Songea ambapo waliona ni vyema waweke mpango wa kununua gari lao, ili baadaye liweze kuhudumia wakazi wa mji huo kwa gharama nafuu pale wanapohitaji huduma.

“Lengo letu ni kuendelea kuboresha huduma ndani ya mji wetu kuwa katika hali nzuri ya usafi, kwa kuhakikisha tunasogeza miundombinu husika karibu na wananchi, waweze kupata huduma kwa urahisi pasipo usumbufu wa aina yoyote ”, alisema Yapesa.

Kadhalika naye Ofisa afya wa mji huo, Felix Matembo alifafanua kuwa utawekwa utaratibu mzuri juu ya matumizi ya gari hilo na baadaye watatoa matangazo kwa wananchi, ili waweze kujua lini litaanza kutumika na wachangamkie fursa iliyopo ya matumizi ya mtambo huo wa kunyonya maji taka.

Pamoja na mambo mengine, Matembo aliongeza kwa kuwataka wakazi waishio katika mji wa Mbinga kuzingatia suala la usafi hasa katika kipindi hiki cha masika ili kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu ambacho hutokana na mazingira kuwa machafu.

Alisema kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu wa masuala ya usafi katika mji huo, kamwe hatakubali kufumbia macho jambo hilo, badala yake anataka kuona watu wanazingatia usafi, kinyume na hapo ameapa kwamba atakayekamatwa anakiuka taratibu husika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 50,000 au kufikishwa Mahakamani.

No comments: