Sunday, November 29, 2015

NDUGU TAMBUA NAMNA YA KUKATA RUFAA


Na Bashir Yakub,

UNAPOSHINDWA kesi  sio  mwisho  wa kusaka  haki. Hii  ni  kwasababu  kushindwa  kesi  kunatokana  na  sababu  nyingi. Si  kweli  kwamba  kwakuwa  umeshindwa  kesi  katika  Mahakama  fulani  basi  maana  yake  ni  kuwa  ulikuwa  huna  haki.

Yawezekana  kabisa  haki  ilikuwa  yako  isipokuwa  umeshindwa  tu  kutokana  na  sababu  nyingine  za  kiutaratibu na  kimbinu (procedures & technicalities). Pia  waweza  kuwa  umeshindwa  kutokana  na  uwezo  mdogo  wa  kujieleza  na kushindwa  kugusa  nukta  muhimu  ambazo  kimsingi  ndizo  zilizokuwa zinabeba   shauri  lako. 

Lakini  pia  waweza  kuwa  umeshindwa  kwasababu  ya  hila  na  mbinu  chafu. Na  hii  wakati  mwingine  huwahusisha  hata  waamuzi yaani Mahakimu  na  majaji.  Basi  ifahamike  kuwa  ni  sababu  hizi   zilizopelekea  kuwepo  utaratibu  wa  rufaa  ili  yule  anayehisi  kutotendewa  haki  aende mbele  ili  kuona  kama anaweza  kupata  haki  yake  huko.

CHAWATA MBINGA YA MUUNGA MKONO MAGUFULI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa Ruvuma kimesema, ifikapo siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Desemba 3 mwaka huu wilaya ya Mbinga itafanya maadhimisho hayo, kwa kuwapatia walemavu wake mahitaji mbalimbali na sio kufanya sherehe kama ilivyozoeleka katika miaka iliyopita.

Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Martin Mbawala alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu juu ya mikakati ya kuwasaidia walemavu na kuwainua kutoka katika umaskini, ambao umekithiri miongoni mwao.

Alisema kuwa kufanya hivyo ni kuunga mkono agizo lililotolewa na Rais John Magufuli kwamba, hakuna sababu ya msingi ya watu kufanya sherehe ya kupika vyakula na kulipana posho kwa maadhimisho ya sherehe mbalimbali, bali fedha husika zikatumike katika shughuli za kimaendeleo.

Friday, November 27, 2015

WAZIRI MKUU MAJALIWA AVAMIA BANDARINI AAMRISHA KUKAMATWA KWA MAOFISA TRA NA WENGINE KUFUKUZWA KAZI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akikabidhi leo orodha ya makontena yaliyopotea bandarini na ambayo TRA haina taarifa zake.


Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo ameamuru kukamatwa kwa Maofisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato hapa nchini (TRA) na wengine kufukuzwa kazi, baada ya kufanya ziara ya kushitukiza bandarini Jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Waziri Mkuu, imefuatia baada ya kukuta madudu ambayo hakuyafurahia na yanadaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wa TRA.

Maofisa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, ili Jeshi la Polisi lianze kazi ya kuwashughulikia wametakiwa pia kusalimisha hati zao za usafiri.

Utekelezaji huo umekuja baada ya kubainika kwamba, kuna makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 80 ambayo data za Mamlaka ya bandari (TPA) inazo, lakini katika mtandao wa TRA hayaonekani.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGANA NA LORI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JOVIN Ndunguru (40) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lukanzauti kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha kugongana uso kwa uso na lori ambalo lilikuwa katika mwendo kasi.

Mihayo Msikhela.
Taarifa za tukio hilo zinaelezwa kuwa dereva, Kanisius Ndunguru (32) mkazi wa Mbinga mjini, aliyekuwa akiendesha lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 242 DBL aligongana na pikipiki hiyo, yenye namba T 432 CAN aina ya Fekon akiwa kwenye kona kali kijijini humo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na marehemu huyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 25 mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana katika kijiji cha Kihulila kata ya Kilimani, barabara ya kuelekea Mbamba bay mjini hapa.  

WANUSURIKA KUPOTEZA MAISHA BAADA YA KUNYWA KINYWAJI KINACHOSADIKIWA KUWA NA SUMU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATU watano akiwemo na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja, ambao ni wakazi wa kijiji cha Mapipili wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamenusurika kupoteza maisha, baada ya kunywa kinywaji ambacho kinasadikiwa kuwa na sumu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa watu hao walikunywa kinywaji aina ya togwa wakati walipokuwa shambani wanalima.
 
Msikhela alifafanua kuwa tukio hilo, lilitokea Novemba 20 mwaka huu majira ya mchana baada ya kunywa kinywaji hicho walianza kujisikia vibaya, ambapo walikuwa wanaharisha na kutapika.

Wednesday, November 25, 2015

WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MALARIA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JAMII wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa kuhakikisha inachukua tahadhari mapema juu ya ugonjwa hatari wa malaria ambao unatajwa kuongoza kuwaua watu wengi, hapa nchini.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo, Adela Mlingi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake ambao walitembelea  Hospitali ya wilaya  ya Mbinga kujionea mkakati wa serikali katika kudhibiti magonjwa hatari ikiwemo malaria, kipindupindu, maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), vifo vya akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. 

Mlingi alisema kulingana na ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo, jamii inapaswa kutambua kwamba ni wajibu wao kuchukua  tahadhari  ya magonjwa hayo mapema, badala ya kuiacha serikali peke yake ambayo kwa upande wake imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana nayo kwa kutafuta dawa na vifaa tiba. 

Sunday, November 22, 2015

HALMASHAURI MBINGA YAFANYA VIZURI ELIMU YA MSINGI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imefanikiwa kuvuka lengo katika upimaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa asilimia 19.23 katika kipindi cha mwaka huu kwa ufaulu wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya   kidato cha kwanza, mwaka wa masomo 2015/2016.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Hayo yamebainishwa na Ofisa elimu ya msingi wa wilaya ya Mbinga, Samweli Komba kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Venance Mwamengo ambapo ufaulu huo umeongezeka kutoka aslimia 57 ya mwaka 2014  hadi kufikia asilimia 76 mwaka huu. 

Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa mikakati thabiti iliyowekwa na idara ya elimu ya msingi wilayani humo, kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi  asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia darasa la kwanza hadi la darasa la saba jambo ambalo mpaka sasa limefanikiwa katika utekelezaji wake. 

Komba alisema mwaka 2014, shule zilizofanya mtihani wa  Taifa kumaliza darasa la saba zilikuwa 217 ambapo jumla ya wanafunzi 7,561 walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,303  sawa na asilimia 56.92 walibahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari. 

MBINGA WAFANIKIWA AKINA MAMA WAJAWAZITO KUJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA



Na Muhidin Amri,
Mbinga.

WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, imefanikiwa kuongeza kiwango cha  akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya na Hospitali, kutoka asilimia 76 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 90  mwezi Juni mwaka huu.

Mbali na hilo, pia kiwango cha wateja wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango nacho kimezidi kuongezeka, kwani hivi sasa idadi ya wazazi wanaopata huduma hiyo imefikia asilimia 105 kutoka asilimia 33, mwaka 2013 na asilimia 85 kwa mwaka 2014. 

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.
Hayo yamebainishwa  na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa akizungumza  na mwandishi wa habari hizi juu ya kuimarika kwa huduma ya akina mama wajawazito wilayani humo na mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya ukimwi (VVU)  kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kabla na baada ya kujifungua. 

Ngaga alisema, idadi ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vimepungua kutoka vifo  169 sawa na vifo 10/1000 mwaka 2013 hadi kufikia vifo 84 ambavyo ni sawa na vifo 7/1000 na mpango uliopo ni kumaliza kabisa vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua akina mama hao, kwani baadhi yake vinatokana na uzembe wa mama kushindwa kuwahi hospitali mapema. 

WATOTO WATEKETEA MOTO BAADA YA MAMA YAO KUWAFUNGIA NDANI YA NYUMBA



Na Steven Augustino,
Songea.

WATU watatu wamefariki dunia, katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika kijiji cha Madaba kata ya Mahanje wilaya ya Songea na kata ya Makambi Manispaa ya Songea, hapa mkoani Ruvuma.

Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa matukio yote yalitokea November 16 mwaka huu na kwamba tukio la kwanza lilitokea kijiji cha Madaba, kata ya Mahanje ambapo watoto wawili walikutwa wakiwa wameungua moto na miili yao kuteketea kabisa.

Mihayo Msikhela, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma.
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa tukio hilo la watoto kuungua moto, lilisababishwa na mshumaa ambao waliwashiwa na mama yao mzazi ambaye wakati tukio hilo linatokea alikuwa kwenye sherehe za kushangilia ushindi wa Diwani wa kata Mahanje, Stephano Mahundi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika November 16 mwaka huu.

Msikhela aliwajata marehemu hao kuwa ni, Happy Mgani (4) na Chesco Mhagama (2) na kwamba mama huyo ambaye hakutaka kumtaja jina lake, yupo chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano zaidi.

WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUGONGA MTAMBO WA KUJENGA BARABARA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU watatu wamefariki dunia katika ajali ya pikipiki, baada ya kugonga mtambo wa kujenga barabara (ROLA) ambao ni mali ya kampuni ya Sino Hydro inayojenga barabara kwa kiwango cha lami, kutoka Tunduru mjini kuelekea katika tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Mashuda wa tukio hilo, walisema kuwa  ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Muhuwesi wilayani humo ambapo Diwani wa kata ya Muhuwesi,  Nurdini Mnolela aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ajali hiyo ilitokea Novemba 15 mwaka huu wakati watu hao wakiwa wanatokea kijiji cha Majimaji kurejea kijijini kwao Muhuwesi.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, wa pikipiki waliyokuwa wakiendesha ambayo ni aina ya Sunlg yenye namba za usajili T 317 CUC mali ya  marehemu Ahamad Athuman (30) hali ambayo, ilimfanya ashindwe kuimudu na hatimaye kugonga mtambo huo.

MAGUFULI AOMBWA KUINGILI KATI MIGOGORO YA WAFUGAJI TUNDURU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAFUGAJI jamii ya Kisukuma, wanaoendesha shughuli zao za ufugaji wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamemuomba  Rais wa awamu ya tano, Dokta John  Magufuli, kuwasaidia kudhibiti migogoro ya wafugaji na wakulima ambayo inaendelea wilayani humo.

Hayo yalisemwa na wafugaji hao, katika sherehe ya kumpongeza Dokta Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilizofanyika kwenye kambi yao ya wafugaji iliyopo kijiji cha Masonya wilayani hapa.

Kiongozi wa wafugaji hao Lugwasha Mtegwambuli, alisema kuwa kufumbiwa macho kwa migogoro hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa, imekuwa ikigharimu maisha yao na kuwafanya waishi kama wakimbizi.

“Tunampongeza Dokta Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, tunaimani naye kubwa katika utendaji wake wa kazi ili wananchi aweze kutufikisha katika maendeleo ya kweli”, alisema Mtegwambuli.

Friday, November 20, 2015

WAANDISHI WA HABARI RUVUMA WAASWA

Na Muhidin Amri,
Songea.

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Robert Mageni amewataka Waandishi wa habari katika mkoa huo, kusaidia kutangaza na kuandika fursa mbalimbali zilizopo katika halmashauri hiyo hatua ambayo itasaidia kuvutia watu wengi, kwenda kuwekeza katika jimbo la Madaba.

Mbali na wito huo, Mageni amewahimiza  kuandika habari nzuri zinazohamasisha wananchi kujikita katika shughuli za maendeleo hususani kwa zile zinazofanywa na wakazi wa jimbo hilo, badala ya kuandika au kutangaza habari za migogoro kwani zinaweza kuhatarisha  kuharibu mahusiano yaliyopo kati ya wananchi na serikali yao.

Mageni alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake katika kijiji cha Madaba, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mahanje  ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephano Mahundi, aliibuka mshindi dhidi ya mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hans Mlelwa.

HAWATAKI KUONA BENDERA ZA CHADEMA ZIKIPEPEA MAHANJE

Na Mwandishi wetu,
Songea.

WANACHAMA 17 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kijiji cha Mahanje jimbo la Madaba wilayani Songea, wamekikimbia chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichoeleza kutofurahishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais katika maeneo mengi hapa nchini licha ya watu wengi kuonekana kukiunga mkono chama hicho.

Edward Lowassa.
Wanachama hao, mbali na kurudisha kadi pia waliamua kuchoma  moto bendera za CHADEMA kwa madai kwamba hawataki tena kuona bendera zake zikipepea kwa sababu zinaweza kuwarudisha,  tena katika Chama hicho.

Mbali na hilo walisema chama hicho licha ya umaarufu wake kisiasa, hata hivyo hakina sera nzuri wala mikakati thabiti inayoweza kukifanya kushinda kwani wagombea wake wengi, ambao wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali hawana uwezo wa kuongoza wananchi ikilinganishwa na wale wanaopitishwa na CCM.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, John Mlelwa alisema wameamua kujiunga na CCM ili kuungana nao  katika mkakati wa kuleta maendeleo ya wananchi kwani tayari hata mgombea wake wa urais, Dokta John Magufuli kwa kipindi kifupi alichokuwa madarakani ameonesha kwa vitendo,  kupigania maisha ya Watanzania hasa wale wa kipato cha chini.

MAHANJE CCM WAIBUKA KIDEDEA

Na Muhidin Amri,
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimeibuka kidedea baada ya mgombea wake wa udiwani katika Kata ya Mahanje jimbo la Madaba wilayani humo, Stephano Mahundi kufanikiwa kushinda katika kiti hicho baada ya kumshinda mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hans Mlelwa.

Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika mwezi uliopita, baada ya kukosekana kwa karatatsi za kupigia kura kwa nafasi ya udiwani, hata hivyo katika nafasi ya ubunge na rais uchaguzi uliendelea kama uilivyopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi kata ya Mahanje, Kanisius Lingowe alimtangaza mgombea huyo wa CCM kuwa mshindi baada ya kufanikiwa kupata kura 946, dhidi ya mgombea wa CHADEMA Hans Mlelwa aliyeambulia kura 487 ambaye hata hivyo, hakuwepo katika chumba cha kutangaza matokeo hayo.

RUVUMA WAPONGEZA UTEUZI WA KASSIM MAJALIWA KUWA WAZIRI MKUU

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Muhidin Amri,
Songea.

BAADHI ya wananchi katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefurahishwa na uteuzi wa Mbuge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa kuwa Waziri mkuu wa Tanzania, katika serikali hii ya awamu ya tano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa, walisema kuwa Majaliwa ndiye mtu sahihi anayefaa  kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wa kazi zake alipokuwa Naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.

Mmoja wa wakazi hao, Thomas Komba alisema ni mtu ambaye ataendana na kasi ya Rais Magufuli lakini pia wakati wote amekuwa kiongozi mwadilifu na mchakapakazi hodari, ambaye hana makundi.

Thursday, November 19, 2015

UCHAMBUZI: NALIONA ANGUKO LA BENEDICT NGWENYA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TANGU kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere kilipotokea katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London nchini Uingereza, hatuna haja ya kurudia ni kiasi gani Watanzania, Afrika na dunia kwa ujumla wake, walivyoguswa na kifo hicho kila mmoja wao kwa nafasi yake, bali itoshe kusema kwamba ulikuwa ni msiba wa dunia.

Licha ya machungu yaliyopatikana kutokana na kifo hicho, Watanzania tunayo faraja kubwa kwa sababu mambo karibu yote, aliyoyapiga vita Mwalimu Nyerere katika uhai wake ili kuleta haki na ukombozi kamili kwa Watanzania, yameleta matunda yaliyotarajiwa.

Benedict Ngwenya.
Mambo hayo ni ukoloni, ukoloni mamboleo na kila aina ya ubaguzi, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi, dini, ukabila na jinsia, rushwa na maadui watatu wakubwa aliowatangaza baada ya kupata Uhuru mwaka 1961.

Maadui hao ni umasikini, ujinga na maradhi. Kwa kuyasoma kwenye kumbukumbu mbalimbali na kuyasikia kwenye vyombo vya habari kwa maana ya magazeti, redio, televisheni na kwenye mitandao ya kijamii hotuba zake zinaishi kwa sababu zinagusa moja kwa moja, yanayotukabili Watanzania hivi sasa kama vile anatushuhudia.

Hotuba hizo zinaishi, kiasi kwamba watu makini wanafarijika ingawaje kwa wale ambao hotuba hizo zinawagusa kutokana na matendo yao machafu ndani ya jamii, wanatamani wangevifungia vyombo vya habari husika, visiendelee kutangaza taarifa hizo.

Alikuwa anayazungumza kuhusu ubaya wa rushwa na namna ya kumpata kiongozi bora sifa zinazotakiwa awe nazo, bila kupotosha maneno na kwa msisitizo unaostahili na lugha sanifu, kiasi kwamba ni kichaa peke yake anaweza kujifanya hasikii au haelewi.

Katika hili sitachelea kuzungumzia juu ya sakata la kumpata mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo wanambinga tunataka liendeshewe kwa amani na utulivu pasipo kujengeana vitisho na dharau.

Benedict Ngwenya ambaye ni Katibu wa siasa na uenezi katika mkoa huo, pia ni Diwani mteule wa kata ya Mpepai ambaye anasubiri kuapishwa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa,………. naweza kusema sasa anashangaza umma.

JE WAJUA SHERIA INARUHUSU KUTENGANA BILA TALAKA ?


Na Bashir Yakub,

KAWAIDA wanandoa  wengi  wanapoingia  katika  migogoro  moja  ya  jambo  wanalokimbilia  kama  jawabu  la mgogoro  ni  talaka.  Kwa  misingi  ya  ndoa  za  kiislamu  talaka  huruhusiwa tofauti  na  misingi  ya  ndoa  za  kikiristo  ambazo talaka  huwa  haziruhusiwi. Hata kama  ndoa  ni  ya  kikristo  ambayo hairuhusu  talaka linapokuja  suala  la  Mahakama  basi  hata  ndoa  hizo  nazo  hutolewa  talaka.  Ieleweke  kuwa kwa  mujibu  wa  sheria  ya  ndoa ya mwaka 1971  suluhu  ya  kumaliza  utata  katika  ndoa  si  talaka  tu.

Na hii ni kutokana  na  umuhimu  wa  ndoa.  Katika  hili sheria ya  ndoa imetoa  chaguo  jingine  ambalo  mtu  anaweza  kulitumia  kama  mbadala  wa  talaka. Hili  linahusu  kutengana  kama  tutakavyoona.

1.KUTENGANA  KISHERIA.

Kutengana   kwa  mujibu  wa  sheria  ni  hatua ambayo  watu  wawili  mwanamke  na  mwanaume  walio  katika  ndoa halali  huamua kutoshirikiana  katika  mambo kadhaa ya  kindoa  huku  ndoa  ikihesabika kuwa  haijavunjika. Katika  hili kinachositishwa ni baadhi ya  haki  na  wajibu  wa  kindoa. Lakini kusitishwa  kwa  wajibu  na  haki    hizo  hakuhesabiki kuwa  kumevunja  ndoa.

DOKTA TULIA NAIBU SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Dokta Tulia Mwansasu.


BUNGE la Jamhurio ya Muungano wa Tanzania, limepitisha jina la Dokta Tulia Mwansasu kuwa Naibu Spika wa Bunge, kwa kura 250 sawa na asilimia 71.2 dhidi ya mpinzani wake, Magdalena Sakaya aliyepata kura 101 sawa na asilimia 28.8.

Idadi ya Wabunge inayotakiwa ni 394, waliosajiliwa 369, akidi ni 184 na waliohudhuria ni 351 na hakukuwa na kura iliyoharibika.

MAJALIWA NDIYE WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Kassim Majaliwa.

HATIMAYE Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muda mfupi uliopita limepitisha jina la Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa serikali ya awamu ya tano baada ya jina lake kupelekwa Bungeni na Rais wa Tanzania, Dokta John Magufuli.

Majaliwa amepitishwa kwa kura 258 sawa na asilimia 73.5 ya kura zote za ndio.

Tuesday, November 17, 2015

KATIBU WA SIASA NA UENEZI MKOA WA RUVUMA ALALAMIKIWA NA WAGOMBEA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MPASUKO mkubwa huenda ukajitokeza na kukikumba Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia Katibu wa siasa na uenezi wa mkoa huo, Benedict Ngwenya kuonekana wazi akiweka mikakati ya kupanga safu za wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga wilayani humo.

Kigogo huyo wa CCM ambaye pia naye ameomba kugombea nafasi hiyo, anadaiwa kupita katika maeneo mbalimbali mjini hapa na kuwatisha baadhi ya wagombea wenzake kwamba, yeye ndiye mwenye uwezo wa kuongoza nafasi hiyo na sio mwingine.

Kufuatia kuwepo kwa malalamiko hayo, imeelezwa kuwa kitendo hicho kinachofanywa na Ngwenya, ni utovu wa nidhamu ndani ya chama ambapo viongozi wenye mamlaka ya uteuzi majina ya wagombea wa nafasi hiyo ngazi ya mkoa, endapo hawatazingatia taratibu husika huenda kukatokea mpasuko mkubwa kwa madiwani wanaotarajia kuunda Halmashauri hiyo mpya, ya mji wa Mbinga.