Sunday, October 4, 2015

MGOMBEA URAIS ACT ASEMA MAENDELEO YALIYOPO YANATOKANA NA JITIHADA ZA VYAMA VYA UPINZANI

Anna Mghwira mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hapa nchini. 
Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kufanya mabadiliko kwa kuchagua wagombea kutoka vyama vya upinzani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu, ili waweze kuwaletea maendeleo yenye kasi ya ajabu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Mgombea urais, Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Anna Mghwira alisema hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi ambao walijitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Baraza la Idd mjini hapa.

Aidha mgombea huyo alipokuwa akizungumza na wananchi hao, aliahidi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa akidai kwamba lengo lake kuondoa chokochoko zilizopo, na mitafaruku ambayo baadaye inaweza kuleta mapigano (Vita) miongoni mwa jamii.

Mghwira alisema endapo atafanikiwa hilo, serikali yake itashirikisha viongozi wa vyama vyote vya siasa, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, ya dini, watalaamu na sekta mbalimbali za kijamii.

Alisema serikali yake kwa kufanya hivyo, anaamini makundi hayo yataimarisha utendaji kazi kwa manufaa ya jamii na kulifanya taifa kukua haraka kiuchumi kulingana na rasilimali husika zilizopo hapa nchini, kama vile gesi na mafuta ambazo wananchi wanapaswa kunufaika nazo.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi ambao walijitokeza kumsikiliza katika mkutano huo, mgombea huyo alikuwa akitamba kuwa bila kuwepo kwa vyama vya upinzani nchi hii, isingeweza kupiga hatua kimaendeleo na kufikia hapa ilipo kwa kile alichodai kuwa Chama tawala (CCM ) viongozi wake wamekuwa wakiandaa mikakati ya kuwanyonya watanzania wenye hali ya chini huku matajiri wakiendelea kujineemesha.

Mgombea huyo wa ACT Wazalendo alisema baada ya chama chake kuyabaini hayo, ndiyo maana kimemsimamisha yeye ili aweze kuwakomboa wananchi ikiwemo kuboresha miundombinu ya ukusanyaji kodi ikiwa ndio msingi mkuu wa maendeleo na kuondoa vitendo vya rushwa na ufisadi, ambavyo hudumaza maendeleo ya taifa hili.


No comments: