Friday, October 2, 2015

APANDISHWA KIZIMBANI KWA KUMCHOMA MOTO MTOTO

Na Muhidin Amri,
Mbinga.

MKAZI mmoja ambaye anaishi katika mtaa wa Kipika wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Aneth Nyaku (24) amepandishwa kizimbani katika Mahakama  ya wilaya hiyo, akikabiliwa na shitaka la kumfanyia ukatili mtoto wa miaka 9,  Mary Emmanuel kwa kumchoma moto katika mkono wake wa kulia.

Akisoma  shitaka hilo mbele ya Hakimu mkazi wa wilaya hiyo, Aneth Nyenyema, Mwendesha mashitaka wa Polisi mkaguzi msaidizi, Seif  Kilugwe  aliiambia mahakama kwamba, tukio hilo lilitokea Septemba 13 mwaka huu majira ya asubuhi nyumbani kwa mshitakiwa huyo ambako anaishi na mtoto huyo.

Mwendesha mashtaka huyo alidai Mahakamani hapo kuwa, Aneth alitenda kosa hilo huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria kama ilivyobainishwa katika kifungu cha makosa ya ukatili kwa watoto, kifungu namba 109 (A).


Ilielezwa kuwwa mshitakiwa alimtendea unyama huo mtoto huyo bila kujali umri alionao na kwamba alimchukua Mary, kwa lengo la kuishi naye baada ya Baba yake mzazi kufariki dunia.

Kwa mujibu wa Inspekta Seif alisema, upelelezi wa shauri hilo umekamilika  kwani  mashahidi wapo na wanachosubiri kufika kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.

Hata hivyo Hakimu Nyenyema, alisema dhamana kwa mshitakiwa iko wazi kwa masharti ya kusaini hati ya dhamana ya shilingi milioni moja na wadhamini wawili waaminifu, ambapo mmoja lazima awe mtumishi wa serikali na kwamba mshtakiwa alitimiza masharti hayo na yupo nje kwa dhamana, hadi kesi hiyo itakapoletwa tena Mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa Oktoba 2 mwaka huu.


No comments: