Tuesday, October 6, 2015

POLISI NA JWTZ WAFANIKIWA KUHARIBU MABOMU MAWILI

Na Mwandishi wetu,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wamefanikiwa kuharibu mabomu  mawili, yaliyokutwa katika Kijiji cha Ngwinde kata ya Litola, wilayani Namtumbo mkoani humo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kuwa mabomu hayo yaliharibiwa ili yasiweze kuleta madhara katika jamii, ambapo moja liliharibiwa majira ya saa nne asubuhi na la pili saa sita mchana.

Alisema kuwa katika mabomu hayo, moja lilikuwa aina ya Motor lenye ukubwa wa mm. 82 ambalo lilikutwa chini ya mti na la pili ni  la kurusha kwa Roketi (RPG) lenye ukubwa wa mm. 122 ambalo lilichimbiwa chini ya ardhi.


Alifafanua kuwa Jeshi hilo, lilipata taarifa kutoka kwa viongozi wa kijiji cha Ngwinde kwamba kuna vyuma vimeonekana katika kijiji hicho na wanamashaka kwamba, huenda yakawa ni mabomu.

Kamanda Malimi alisema  siku iliyofuata  baada ya kupokea taarifa hiyo, Polisi kwa kushirikiana na askari wa JWTZ, walifika katika  eneo la tukio na kuyakuta mabomu hayo mawili ambayo yalikuwa katika kijiji hicho.

Malimi alibainisha kwamba, katika uchunguzi wa awali walibaini kuwa eneo walipoyakuta mabomu hayo ni sehemu  ambayo ilikuwa ikitumika kwa ajili ya mazoezi ya Jeshi la Wananchi  wa Tanzania, pamoja na vikosi vingine vya ulinzi na usalama kutoka makao makuu ya Brigedi ya 401 Songea miaka ya nyuma na mpaka mwaka 2012, na kwamba ufuatiliaji wa karibu utafanyika ili kuweza kuona kama kuna masalia mengine ya mabomu.


Kamanda Malimi amewataka wananchi wa mkoa  wa Ruvuma, kuendelea kuwa na moyo wa kutoa taarifa juu ya vitu wanavyovitilia mashaka kwenye maeneo yao na kuwajulisha viongozi wao, wa mitaa na vijiji ikiwemo hata kutoa taarifa katika vituo vya Polisi.

No comments: