Sunday, October 4, 2015

NGAGA: MWALIMU ATAKAYEKUWA MTOVU WA NIDHAMU ATACHUKULIWA HATUA

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

WALIMU  nchini wametakiwa kukataa kugeuzwa wapiga debe na kuwa madalali wa  vyama vya  siasa, badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi kwa kuongeza juhudi ya ufundishaji watoto darasani, hatua ambayo itasaidia kuwaongezea uelewa wanafunzi na kukuza taaluma hapa nchini.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi ngaga alisema hayo, mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua kikao cha siku tatu kwa wakuu wa shule za sekondari kutoka mikoa mitatu ya nyanda za juu kusini Ruvuma, Njombe na Iringa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa katoliki uliopo mjini hapa.

Mbali na hilo, pia amewaonya walimu hao kutotumia maeneo ya shule kufanyia kampeni wanasiasa kwa sababu maeneo hayo, sio rasmi kwa ajili ya shughuli hizo huku akisisitiza kwamba tabia hiyo inawanyima fursa watoto, kupata haki yao ya msingi.


Ngaga alieleza kuwa serikali haikatazi mwalimu kuwa na mapenzi na chama au mgombea fulani, lakini hilo lifanyike mara atakapotoka shule baada ya kutimiza majukumu yake ya kazi.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alifafanua kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua mwalimu yeyote atakayebainika kuwa ni mtovu wa nidhamu, kutokana na kuingia katika siasa na kuacha majukumu yake ya msingi aliyopewa na serikali kwa ajili ya kutumikia wananchi.

Aidha amewaagiza wakuu wa shule hizo, kwa kushirikiana na kamati zao za shule kwenye  maeneo yao kuhakikisha wanawabana wazazi na walezi, ambao wamekuwa kikwazo kwa kutopeleka watoto wao shule ili kuweza kupunguza tatizo sugu la utoro shuleni.

Ngaga alisema baadhi ya shule zina idadi ndogo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo, tofauti na idadi halisi ya walioandikishwa kuripoti shuleni huku akisisitiza kuwa muda umefika sasa,  kwa walimu na kamati zao za shule kuwasaka watoto hao waliokacha kwenda shule ili  waweze kuendelea na masomo.

Aliongeza kuwa kama kutakuwa na mahudhurio mazuri, kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, hata ufaulu wake huongezeka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa shule za Sekondari (TAHOSA) Ponsian Ngunguvu, alisema lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu hasa katika mambo ya utawala, tatizo la migogoro kazini na kuziunganisha shule zote za sekondari kuwa kitu kimoja, ili kuweza kupanga mikakati ya pamoja katika kuinua kiwango cha taaluma kwa shule husika.

Ngunguvu alibainisha kuwa kufuatia kuwepo kwa umoja huo, tayari wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwa na mitihani ya pamoja, katikati na mwisho wa muhula na kuboresha mazingira ya shule zao.


Hata hivyo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha, miongozo ya umoja wa michezo kwa shule za sekondari umiseta na kukosekana kwa hatimiliki kwa shule nyingi, jambo ambalo linasababisha migogoro ya mara kwa mara katika jamii. 

No comments: