Sunday, October 4, 2015

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA SEKTA YA AFYA

Na Muhidin Amri,
Namatumbo.

SERIKALI imesema, itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa  nyumba za wauguzi, madaktari na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuwavutia  watumishi wa idara  ya afya, kupenda kufanya kazi wakiwa katika mazingira mazuri na waweze kutekeleza majukumu ya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa uchaguzi kwa viongozi wa chama cha wauguzi mkoani humo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Faraja uliopo mjini hapa.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho.
Alifafanua kuwa serikali inatambua matatizo yanayowakabili wafanyakazi wa idara hiyo, ambapo itaendelea kuboresha mazingira yao ikiwemo pia mishahara na maeneo ya kufanyia kazi zao.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa bado serikali inaendelea kuajiri watumishi wengi mwaka hadi mwaka, sambamba na ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali ili kukidhi mahitaji husika ya watanzania kwa kila  mkoa, wilaya, kata na vijiji ikiwa ni lengo kwamba wananchi wake waweze kupata huduma ya matibabu kwa urahisi.


Nalicho alisema kazi ya uuguzi  inahitaji moyo wa uzalendo na kujituma, hivyo watumishi wake wanapaswa kujiangalia kuhusu utendaji wa kazi zao na kuwafichua wenzao, ambao wanakwenda kinyume na taaluma hiyo jambo ambalo linahatarisha usalama wa maisha ya binadamu.

Kutokana na hilo, amewahimiza pia kutekeleza wajibu wao  kwa kufuata maadili ya kazi zao pamoja na miongozo mbalimbali iliyowekwa na Wizara ya afya na ustawi wa jamii, kitendo ambacho kitasaidia kupunguza malalamiko ya hapa na pale kutoka kwa wananchi.

  

No comments: