Wednesday, October 28, 2015

MEYA MANISPAA YA SONGEA ASHINDWA KUTETEA KITI CHAKE



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ALIYEKUWA Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Charles Mhagama katika kipindi kilichopita ameshindwa kutetea kiti chake cha udiwani kata ya Matogoro kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa hiyo, baada ya mgombea udiwani wa kata hiyo kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Alawi Kawelea, kuibuka mshindi.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea, Raphael Kimari alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema CCM kimefanikiwa kushinda kata 16, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshinda kata 4 na CUF kimeshinda kata 1 ambapo jimbo hilo lina jumla ya kata 21.

Charles Mhagama.
Kimari aliwataja washindi wa Chama Cha Mapinduzi na kata zao kwenye mabano, kuwa ni Oddo Mbunda (Mjimwema), Festo Mlelwa (Seedfarm), Mshawej Hassan (Subira), Maurus Lungu (Mletele), Yobo Mapunda (Lilambo), Lotari Mbawala (Mshangano), Cresensia Kapinga (Ndilimalitembo) na Osmund Kapinga wa kutoka kata ya Mwengemshindo.

Aliwataja wengine kuwa ni Wilbart Mahundi (Ruhuwiko), Ismail Aziz (Misufini), Shaib Kitete (Mjini), Hussein Abukadi (Majengo), George Oddo (Lizaboni), Golden Sanga (Bombambili), Izack Lutengano (Msamala) na Mussa Mwakaja kata ya Mateka.


Msimamizi huyo alizitaja kata ambazo CHADEMA kimeshinda kuwa ni Rashid Msuso (Ruvuma), Mussa Ndomba (Tanga), Martin Mlata (Matarawe), Seneta Yatembo (Mfaranyaki) na Alawi Kawelea kata ya Matogoro ambaye ameshinda kiti hicho kupitia Chama cha Wananchi CUF.

Hata hivyo alisema kwamba mpaka sasa, hajapokea malalamiko yoyote kuhusiana na matokeo hayo na kwamba hali hiyo inaonesha kuwa Tume ya uchaguzi imetenda haki kwa wagombea wote, na wananchi wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua kiongozi ambaye wanamtaka.

No comments: