Friday, October 2, 2015

MGOMBEA CHADEMA KUWATATULIA WANAMKAKO MATATIZO YAO

Na  Julius Konala,
Mbinga.

MGOMBEA udiwani kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Mkako wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gabriel Mwinuka amesema kuwa endapo wananchi wa kata hiyo watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao, atahakikisha anapambana kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii katika kata hiyo, ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama.

Mwinuka aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, akielezea mipango na mikakati  yake mbalimbali, atakayoitekeleza katika kuwatumikia wananchi pindi atakapochaguliwa kuwa Diwani wa kata hiyo.

Alisema kuwa kata hiyo kwa muda mrefu imekuwa na tatizo la ukosefu wa huduma hiyo muhimu, katika vijiji vya Mkako, Lihale na Kihuruku hali ambayo inawalazimu akina mama kutembea umbali mrefu kufuata maji pamoja na kusababisha wananchi kuugua homa za matumbo.


Alieleza kuwa, yeye kwa kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wanaounda Umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) watatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, ikiwemo kuboresha miundombinu yote ya maji, barabara, ujenzi wa nyumba za wahudumu wa afya na walimu.

Kadhalika alisema katika uongozi wake, atahakikisha anaunganisha nguvu za wananchi na Halmashauri katika kujenga kituo cha afya kwenye kata hiyo kwa madai kuwa wananchi wanapata tabu ya kutembea umbali mrefu, kufuata huduma kwenye gereza la kitai pindi wanapougua ambapo alisema wakati mwingine matatizo yanapotokea usiku hasa kwa akina mama wajawazito inakuwa ni vigumu kupata huduma muhimu ya matibabu.

Mgombea huyo pia alidai kuwa katika kipindi atakachokuwepo madarakani atahakikisha anajitahidi kutatua changamoto  ya muda mrefu, ya ujenzi wa daraja la mto Ruvuma linalounganisha kijiji cha Lihale wilayani Mbinga na kijiji cha Lusonga kilichopo katika wilaya ya Songea, kwa madai kuwa kukosekana kwa daraja hilo kunawakwamisha wananchi kusafirisha mazao yao ya mahindi, kwa ajili ya kupeleka kusaga unga kwenye kiwanda cha masista wa Chipole.


Mwinuka amewaomba wananchi hao wamchague siku ya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais ifikapo Oktoba 25 mwaka huu ili akashirikiane na viongozi wanaounda Umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) kwa malengo ya kuwatatulia matatizo yanayowakabili, ikiwa pamoja na kufuta michango ya shule isiyo ya lazima pamoja na kuondoa vizuizi ambavyo vimekuwa kero kwa wakulima wakati wa kusafirisha mazao yao kutoka shambani.

No comments: