Tuesday, October 13, 2015

MGOMBEA UBUNGE TUNDURU KUSINI AFANANISHWA NA JEMBE


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAPENZI na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, wamemfananisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Daimu Mpakate  kuwa ni sawa na jembe na pembejeo za kilimo, ambavyo wamekuwa wakivitabikia kwa muda mrefu jimboni mwao.

Wananchi wenye  bendera za chama hicho, walikuwa na mabango yenye kubeba ujumbe  wa aina mbalimbali ambao ulikuwa ukimuunga mkono mgombea huyo, huku  wakiimba  nyimbo za kumpongeza kuchaguliwa kwake, kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho.

Hayo yalibainishwa kwa vitendo kutokana na wananchi hao, pale walipojitokeza kwa wingi huku wakiwa wameinua mabango hayo ambayo yalikuwa na ujumbe wakumpa moyo mgombea, kwamba watamchagua kwa kumpatia kura zaidi ya asilimia zaidi ya 80.


Baadhi yake yalikuwa na ujumbe yakisema, “Mpakate  umethubutu, unaweza, tunakukubali, tunakuamini, ukitaka mabadiliko chagua CCM, tunaimani  na Mpakate kero yetu ya zao la korosho itakwisha, Mpakate wewe ni jembe, pembejeo za kilimo zitafika kwa wakati”.

Aidha toka kampeni za kuwania nafasi hiyo, tokea zianze kutimua vumbi  katika jimbo hilo kwa mara ya kwanza Mpakate alipata mapokezi makubwa yaliyoweza kufananishwa na gharika, kutokana na idadi  kubwa ya wananchi waliojitokeza kumlaki na kumsikiliza kwanye mkutano wake wa kampeni, uliofanyika kwenye viwanja vya mikutano vya makaoni vilivyopo katika kijji cha Lukumbule wilayani Tunduru mkoani hapa.

Katika mkutano huo mgombea huyo, aliwashukuru wananchi waliojitokeza na kuvunja rekodi ya vyama vingine vya siasa wilayani humo, kwamba havijawahi kupata umati mkubwa wa watu katika kampeni zao na kwamba hizo ni salamu kuwa jimbo lake halihitaji viongozi wa upinzani.

Kufuatia hali hiyo Mpakate aliwataka wanchi wa jimbo la Tunduru Kusini, kupuuza kelele za wapinzani na akawataka kujitokeza kwa wingi kumchagua mgombea urais wa CCM, mbunge na diwani  ili waweze kuwaletea maendeleo ya kweli na kwamba  yeye ni mtetezi wa wanyonge, na anazifahamu kero zinanazo wakabili wananchi wa jimbo hilo. 

Mpakate alitamba kuwa Chama cha mapinduzi, endapo kitachukua nafasi ya ushindi ya kuongoza  katika kipindi cha miaka mitano ijayo kitajikita zaidi katika kuimarisha miundombinu ya elimu, kilimo, afya, maji na michezo ambavyo vimeainishwa kusimamiwa  katika ilani ya chama chake katika kipindi hicho.

Naye Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Tunduru, Hamis Kaesa aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi  siku ya kupiga kura na kuwachagua wagombea waliosimamishwa na chama chake, kwa kuwapatia kura nyingi za ndiyo ili waweze kuwaongoza katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano chini ya Dokta John Magufuli.

Kadhalika Mwenyekiti wa Jumuiya ya  wazazi ya CCM wilayani humo, Said Mkandu aliwaasa wananchi wajimbo hilo wasiwachague viongozi wa UKAWA  kwa kile alichodai kuwa wamesambaratika  na hawawezi kuleta maendeleo wilayani humo na Taifa kwa ujumla.

Vilevile kiongozi kimila wa makabila ya Wayao kutoka kijji cha Lukumbule,  Mwenye  Kanyinda  alimhakikishia mgombea ubunge katika jimbo hilo, Mpakate kuwa wananchi watampigia kura nyingi.


Aidha Mwenye Kanyinda alimuomba mgombea huyo, atakapoingia madarakani  ahakikishe katika tarafa ya Lukumbule anawajengea  kituo kidogo cha Polisi  ili waweze kuishi kwa amani, tofauti na ilivyo sasa ambapo wamekuwa wakiishi kwa mashaka kutokana na kuwa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

No comments: