Friday, October 16, 2015

TUNDURU WAISHUKURU SERIKALI AWAMU YA NNE



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANUFAIKA katika mradi wa uhawilishaji fedha, kaya maskini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa kubuni na kuwapelekea mradi huo.

Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea fedha kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, kondoo, kuku, kanga, bata, matibabu pamoja na kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.

Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye mahojiano maalum na mwandishi wetu ambaye alitembelea vijiji vya Mbesa, Nalasi, Mchoteka, Tunduru mjini  na Namasakata wilayani humo.


Wakifafanua maelezo yao kwa nyakati tofauti, wanufaika hao walisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo hadi sasa baadhi yao wameweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kujikwamua na umaskini waliokuwa nao, ikiwemo kupeleka watoto wao shule.

Mohammed Ponera wa kijiji cha Mbesa na Sheila Salum kwa nyati tofauti walidai kuwa, mradi huo umewawezesha kumiliki wastani wa mbuzi wanne hadi sita kila mmoja wao na kuanza kuuaga umaskini uliokithiri miongoni mwao kwa muda mrefu.

Wengine waliohojiwa katika ufuatiliaji wa mradi huo, ni pamoja na Mwanahawa Daimu wa kijiji cha Mbesa, Siwema khalfan wa  kijiji cha Nalasi, Siwema Rashid wa Kijiji cha Mchoteka  na Mohammed Alifa wa Kijiji cha Nakayaya walisema kuwa mradi huo umewanufaisha kutokana na kuanza kufuga kuku na bata ambao wameanza kuuza mazao yatokanayo na mifugo hiyo.

Walibainisha kuwa hapo awali hawakuwa na uwezo wa kufuga hata kifaranga kimoja cha kuku, hivyo mfuko huo umewafanya kila mmoja wao kumiliki kati ya kuku 40 hadi 60, bata, kati ya 50 na 70 pamoja na kanga ambao walidai kuwa na idadi tofauti jambo ambalo linawapa faraja na ni hatua nzuri kimaendeleo katika maisha yao.

Sambamba na fedha za TASAF kuwasaidia kuanzisha ufugaji huo, pia zimekuwa zikiwasaidia kusomesha watoto wao shule ikiwa ni pamoja na kuwanunulia sare, daftari, kalamu na mahitaji mengine muhimu ya mtoto.

Ayesi Linyomwa wa kijiji cha Namasakata alitoa ushuhuda wake akisema, fedha hizo zimemsaidia kujenga nyumba, anafuga kuku, pamoja na kuendeleza shamba lake la mikorosho ambalo awali lilikuwa lina hali mbaya kutokana na kushindwa kulihudumia.

Mkazi wa kitongoji cha Ajika kijiji cha Mbesa, Chinunga Said naye alisema kuwa pamoja na kuanza kumiliki mbuzi na kuku lakini fedha hizo zilimsaidia kumuuguza kijana wake, ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kichaa.

Wakizungumzia changamoto ambazo wamekuwa wakizipata wakati wa ugawaji wa fedha hizo, baadhi ya wataalamu kutoka TASAF walisema kuwa awali kulikuwa na matatizo ya wateja hao kurukwa na kompyuta jambo ambalo lilikuwa likileta malalamiko ya hapa na pale na sasa limefanyiwa kazi na hakuna tena usumbufu wa aina yoyote ile.

Wawezeshaji kutoka katika mfuko huo wilayani Tunduru, Muhidin  Shaibu na Twaha Nang'onde waliwaasa wanufaika hao kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitatumika kukopeshana fedha bila riba, ili fedha wanazopata ziendelee kuwanufaisha hata baada ya mradi huo kwisha.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Ofisa mshauri na mfuatiliaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri wilaya ya Tunduru, Christian Amani alisema jumla ya shilingi bilioni 2,850,708,702.06 zimelipwa kwa awamu, kwa wanufaika 60,412 waliopo katika kaya 15,012 zilizoainishwa tokea mradi huo uanzishwe.

Kwa mujibu wa takwimu za wanufaika hao, kati yao wanaume 22,412 na wanawake 38,000 ambao kati yao wanapokea ruzuku ya msingi, ruzuku ya masharti ya elimu na afya.

Alisema malipo hayo ni miongoni mwa malengo makuu ya TASAF, awamu ya tatu na lengo ni kuiwezesha jamii kuondokana na umaskini uliokithiri kwa kujenga rasilimali watu, kupitia elimu na afya kwa watoto.

Pamoja na mambo mengine, Amani aliwaasa wanufaika wahakikishe kwamba fedha wanayoipata wanaitumia katika malengo husika na endelevu, ili mradi huo utakapofikia hatua ya mwisho walengwa waendelee kufaidi matunda.

Hata hivyo aliwahakikishia walengwa  hao kuwa, mfuko huo utawasaidia katika mchakato wa kurasimisha vikundi vyao vya uzalishaji mali, ambavyo wamevianzisha pamoja na kuwawezesha kufikia maendeleo kwa kila mnufaika aliyekuwa katika mradi.

No comments: