Friday, October 23, 2015

MWAMBUNGU: PIGENI KURA NA KURUDI NYUMBANI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

YAKIWA yamebaki masaa machache Watanzania kushiriki katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, Serikali mkoani Ruvuma imewataka wananchi wake mkoani humo, Oktoba 25 mwaka huu kushiriki kikamilifu kupiga kura katika kituo husika walichojiandikisha na mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, waondoke na kurudi nyumbani.

Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la Yeboyebo, katika ukumbi wa Songea Club uliopo mjini hapa.

“Nawasihi sana, mkisha piga kura ondokeni katika eneo la kituo na kuwaacha mawakala wa vyama husika wakilinda kura zenu”, alisema Mwambungu.


Aidha Mwambungu aliwasihi madereva hao, wasikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa kufanya matendo maovu au vurugu, siku uchaguzi mkuu utakapofanyika.

“Msikubali kutumika na hiyo ndiyo rai yangu kwenu, nawaomba kapigeni kura kwa utulivu, waepukeni wanasiasa wenye nia ovu ambao hawalitakii mema Taifa hili”, alisema.

Aliongeza kuwa serikali ina mkono mrefu, hivyo kila wakati imekuwa ikitambua nini kinafanyika na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo, kwa lengo la kuepusha vurugu na kulinda amani na utulivu kwa raia wake.

Hata hivyo kwa upande wao, madereva hao wa pikipiki kwa nyakati tofauti walimthibitishia Mkuu huyo wa mkoa kwamba, watazingatia maelekezo aliyowapa na kuhakikisha hakuna vurugu itakayotokea.

No comments: