Friday, October 2, 2015

SIXTUS MAPUNDA AWATAKA WANAMBINGA KUKIPATIA KURA NYINGI CHAMA CHA MAPINDUZI

Sixtus Mapunda ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, hivi karibuni alipokuwa akikabidhiwa Ilani ya utekelezaji ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) na mgombea Urais wa chama hicho hapa nchini, John Magufuli katika viwanja vya CCM Mbinga mjini.
Na Muhidin Amri,
Mbinga.

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Mbinga mjini, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Sixtus Mapunda amewataka wananchi wa jimbo hilo kukipa ushindi mkubwa chama hicho na wagombea wake wa udiwani, ubunge na urais ili kiweze kutimiza ndoto yake ya maisha bora, kwa kila mtanzania.

Mapunda ambaye pia ni Katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho taifa (UVCCM) alisema hayo hivi karibuni, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya soko kuu Mbinga mjini na kusisitiza kuwa CCM ndicho chama chenye sera nzuri na mipango madhubuti ya kimaendeleo.

Amewaomba wakazi wa mji huo, kumchagua kwa kura nyingi Oktoba 25 mwaka huu ili aweze kutimiza ndoto yake ya kimaendeleo na kuleta matumaini mapya kwa wananchi na chama kwa ujumla, hasa kwa wale walioanza kukata tamaa na vitendo vya ufisadi vilivyokuwa vinafanywa na baadhi ya makada wake ambao wamekimbilia vyama vya upinzani, baada ya kuona hawana sifa ya kubaki ndani ya chama hicho.


Mapunda alifafanua kuwa yeye na Chama cha mapinduzi, wanafahamu changamoto zinazowakabili watu wa Mbinga hata hivyo tayari serikali ya CCM imeshaanza kuzipatia majibu huku akitolea mfano wa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Songea hadi Mbinga, yenye urefu wa kilometa 96 ambayo imejengwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Marekani.

Katika Mkutano  huo wa kampeni pia wanachama 20 kutoka CHADEMA, ACT Wazalendo na Chama cha wananchi CUF walirudisha kadi za vyama hivyo na kujiunga na Chama cha mapinduzi, ambapo Mapunda aliwataka wananchi kutokubali kufuata propaganda zinazotolewa na vyama hivyo, kwa kuwa zinalenga kuhamasisha kuleta vurugu na uvunjifu wa amani hapa nchini.

Mbali na hilo, amewataka wananchi wa Mbinga na Tanzania kwa ujumla kuacha mawazo ya kumpigia kura mgombea urais wa Ukawa ambaye anaungwa mkono na vyama vingine vya upinzani, Edward Lowassa kwa sababu kama atakuwa Rais hawezi kuwaletea maendeleo kwani  kila anapokuwa katika mikutano yake ya kampeni, amekuwa ni mtu wa kutoa ahadi nyingi za uongo na zisizotekelezeka badala yake ataangalia jinsi ya kurudisha fedha anazotumia kuwahonga baadhi ya wanachama wa CCM ili wahamie katika vyama vya upinzani.

Mapunda alisema kiongozi mzuri wa siasa ni yule  ambaye hatoi ahadi za uongo kwa wapiga kura wake, bali ni mwenye uwezo na anayejua kero mbalimbali za wananchi ili aweze kuzitatua na kuleta maendeleo katika eneo husika, kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
 

No comments: