Monday, October 12, 2015

MANJORO KUMBWAGA RAMO TUNDURU KASKAZINI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAKATI kampeni za Uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika  Oktoba 25 mwaka huu zikiendelea kushika kasi sehemu mbalimbali hapa nchini, mgombea ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) na Umoja wa Katiba ya Wananchi  (UKAWA) Manjoro Kambili, amesema ataendelea kujiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba anajipatia ushindi mnono na kujinyakulia jimbo hilo, ili aweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Jimbo hilo kwa sasa mgombea huyo, anapambana na Mhandisi Ramo Makani ambaye anapeperusha bendera kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hayo yamebainika kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, ambapo taarifa zinaonesha kuwa Kambili amechukua maamuzi hayo kutokana na kuwepo kwa mgogoro mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM ambao unafukuta chini kwa chini, huku kukiwa na kundi kubwa lililoanza kujitokeza na kumuunga mkono mgombea huyo wa UKAWA.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mgombea huyo wa Ukawa ameanza kuyaita makundi hayo na kuzungumza nayo katika vikao vyake mbalimbali na kufanya makubaliano, ambayo yatamhakikishia kuibuka na ushindi huo.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya viongozi wa makundi hayo ya Chama cha mapinduzi, walikiri hilo kufanyika na kwamba wao wapo tayari kuzungumza na mgombea huyo huku wakiongeza kuwa wanachohitaji awamu hii ni mabadiliko ya uongozi.

Walifafanua kuwa wapo tayari kuzungumza na  mgombea huyo wa upinzani kwa kile walichoeleza kuwa viongozi wa chama chao (CCM) wamekuwa hawasikilizi na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Jimbo hilo, jambo ambalo chama hicho kimetumia mabavu kumteua Mhandisi, Ramo Makani kuwa mgombea Tunduru Kaskazini.

Kutokana hali hiyo hivi sasa mgombea huyo wa CCM, ameshindwa kumaliza tofauti hizo ambazo zinaendelea kumtafuna kila kukicha, na sasa wanachama wake wanasema wataendelea kumpuuza.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyoleta dhahama hiyo, ndani ya Chama cha mapinduzi Mhandisi Ramo alitangazwa kuwa mshindi wa kwanza katika matokeo ya uteuzi wa kuwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tunduru Kaskazini, kwa kupata kura 5,286 jambo ambalo liliwafanya wagombea wenzake kususia na kutosaini, matokeo hayo yaliyompatia ushindi huo kwa madai kuwa aliyachakachua.

Wagombea wengine ambao walichuana na Mhandisi huyo ni Omary Ajili Kalolo alishika nafasi ya pili kwa kupata kura  3,957,  Issa Mohamed Mtuwa alishika nafasi ya tatu kwa kura 2,025, Rashid Mohamed Mandoa kura 1,719, Athuman Salehe Nkinde kura 1,296, Shaban  Richard Uronu kura 942, Hassan Zidadu Kungu kura 687, Michael Augustino Matomora kura 480, Moses Ally Kaluwayo alishika nafasi ya mwisho kwa kupata kura 353.

No comments: