Thursday, October 15, 2015

UWT RUVUMA YA WAASA WANACHAMA WAKE

Na Muhidin Amri,
Songea.

KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Ruvuma, Chiku Masanja amewataka wanawake wa mkoa huo, kuwaunga mkono  wanawake wenzao waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho.

Alisema wanawake wakipata nafasi za uongozi, itakuwa rahisi kwao kuwatetea wanawake wenzao katika vikao mbalimbali vya maamuzi hasa vile vya baraza la madiwani, ubunge na kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli ambazo  zitawawezesha wajikwamue kiuchumi.

Chiku aliyasema hayo jana, wakati  alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya wanawake, kata ya Misufini Manispaa ya Songea mkoani humo kwenye ukumbi wa CCM tawi la mjini, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya umoja wao sambamba na kuwakumbusha juu ya wajibu wa kila mwanamke kushiriki kikamilifu kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Oktoba 25 mwaka huu katika eneo lake analoishi.


Wanawake wakiwa viongozi ni wawakilishi muhimu wa wanawake wenzao, na wanapokuwa kwenye vikao jukumu lao kubwa ni kuhakikisha maslahi ya wanawake yanajadiliwa kwa upana wake, hasa ikizingatiwa kuwa mwanamke ni nguzo kuu ya maendeleo.

Alieleza kuwa UWT inategemewa katika kufanikisha ushindi wa chama tawala, hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanapita kwenye maeneo yao na kuitisha mikutano, ambayo wataelezea kwa kina namna ambavyo serikali inavyotekeleza majukumu yake.

"Wanawake  ni watu muhimu kwa ushindi wa Chama chetu, tumekusanyika hapa ili tukumbushane majukumu ya kila mmoja katika eneo lake na kuhakikisha kwamba chama chetu kinashinda katika uchaguzi kwa ngazi ya udiwani, ubunge na rais”, alisema Masanja.


Hata hivyo alisistiza juu ya umuhimu wa wanawake, kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa ili kusikiliza sera na ahadi za wagombea wake, kwa lengo la kuwa na maamuzi sahihi siku ya kupiga kura na kuwachagua wanawake wenzao walioomba nafasi za uongozi kupitia CCM ili waweze kuchaguliwa.

No comments: