Monday, October 12, 2015

VITUO 216 JIMBO LA PERAMIHO KUTUMIKA KUPIGIA KURA

Mlemavu asiyeeona akisoma mfano wa karatasi ya kupigia kura, wakati wa mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watu wenye ulemavu.
Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JUMLA ya vituo 216 vimetengwa katika jimbo la Peramiho, lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka huu.

Akizungumza na mwandishi wetu, kwa niaba ya msimamizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo Sixbert Valentine, Ofisa uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Furaha Mwangakala, alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika.

Mwangakala alifafanua kuwa katika kila kituo ndani ya Jimbo hilo, kutakuwa na wapiga kura 450 kwa lengo la kupunguza msongamano na kutoa fursa kwa wananchi wote ambao wamejiandikisha, waweze kupiga kura bila kupata usumbufu wa aina yoyote ile.

Alisema kuwa, kufuatia zoezi hilo jumla ya watu 67,334 kwa Jimbo la Peramiho wenye sifa ya kupiga kura wamejiandikisha, miongoni mwao yakiwemo makundi mbalimbali ya wazee, vijana, wanawake kwa wanaume ili waweze kutumia haki yao ya msingi kuwachagua viongozi wao.


Kwa upande wa maandalizi alieleza kuwa yanaendelea vizuri kwa madai kuwa mpaka sasa jumla ya wasimamizi wa uchaguzi 800 wameteuliwa, maboksi ya nyongeza yenye rangi ya bluu 40, meusi 40 na meupe 40 tayari yamekwisha pokelewa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Ofisa uchaguzi huyo aliendelea kuvitaja vifaa vingine vilivyowasili kuwa ni mabango ya hadhari, mabango ya vituo, mabango ya mshale, nyembe za kukatia lakili, betrii za taa, vitabu vya maelekezo kwa watakaosimamia uchaguzi pamoja na fomu kwa ajili ya mafunzo ya wasimamizi wa vituo na makarani.

Mwangakala aliongeza kuwa kwa upande wa makundi maalumu hususan kwa  watu wasioona, tayari wamekwisha waandalia karatasi zao maalumu za kupigia kura pamoja na kuwatengenezea utaratibu mzuri, ambapo pia kundi hilo likiwemo la wazee na walemavu wengine wa aina mbalimbali, akina mama wajawazito nao hawatasimama kwa muda mrefu kupiga kura badala yake watapewa kipaumbele kwanza na wengine watafuata kutekeleza zoezi hilo muhimu.


Hata hivyo baadhi ya wananchi wakizungumza kwa nyakati tofauti, walieleza kuwa wanashindwa kuelewa kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa vyama ambapo wanawaambia wafuasi wao kuwa wakipiga kura lazima wazilinde, huku sheria ya tume inasema kuwa ukisha piga kura  unatakiwa usimame umbali wa mita 100 na vyombo vya dola vinasema ukipiga kura unatakiwa kurudi nyumbani ili kusubiri matokeo, jambo ambalo walisema kuwa wanapaswa kuelimishwa ipasavyo kupitia vyombo vya habari na pale mikutano ya kampeni inapofanyika.

No comments: