Sunday, October 4, 2015

WANAFUNZI SEKONDARI AGUSTIVO MBINGA WAFUNDWA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kutojiingiza kwenye masuala ya anasa kama vile vitendo vya kimapenzi, ambavyo husababisha kukatisha ndoto ya kujiendeleza kimasomo katika maisha yao.

Aidha wakati wote wametakiwa kuonesha dhamira ya kusonga mbele, kwa kujikita zaidi kwenye malengo ya kuongeza elimu kwa faida ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Ushauri huo ulitolewa jana na Khalid Kingi, ambaye ni Katibu msaidizi wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) katika mahafali ya kidato cha nne shule ya sekondari Agustivo iliyopo mjini hapa, ambapo katika sherehe hizo alikuwa akimwakilisha mgeni rasmi Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus Mapunda.

“Ndugu zangu mnahitimu masomo yenu katika kipindi ambacho kina changamoto nyingi, natoa wito kwenu na kwa wengine hapa wilayani ambao wanahitimu kidato cha nne kama ninyi, huko muendako mkapambane na changamoto za ulimwengu huu kwa kuweka malengo ya kuongeza elimu, na kuacha tabia ya kufikiria maisha ya mtaani ambayo yatawafanya mwisho wa siku mjiingize kwenye makundi mabaya”, alisema Kingi.


Pia alipongeza safari za mafunzo kwa vitendo ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, kwa watoto wanaosoma katika shule hiyo, ambayo yamekuwa yakiwajengea uwezo na kuwafanya waweze kufanya vizuri katika masomo yao na mitihani kwa ujumla.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya shule, Makamu mkuu wa shule hiyo Thomas Komba alisema kuwa maendeleo kitaaluma matokeo ya mitihani ya ndani na nje ya wilaya, imekuwa ikileta taswira nzuri ya ufaulu ambapo umekuwa mkubwa kimkoa na Taifa kwa ujumla.

Komba alieleza kuwa matokeo ya mitihani mbalimbali, imeendelea kutia hamasa na kuonesha tumaini bora kwa wanafunzi, wazazi na walezi.

Changamoto wanazokabiliana nazo shuleni hapo, Komba alizitaja kuwa ni upungufu wa vifaa vya maabara kwa masomo ya sayansi, vitabu vya kiada na ziada pamoja na uzio kuzunguka eneo la shule kitendo ambacho kinasababisha baadhi ya wanafunzi kutoroka na kuelekea nje ya eneo la shule, jambo ambalo huchangia kushuka kwa taaluma na nidhamu.


Hata hivyo changamoto nyingine, alisema kuwa baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu na walimu hasa kwa upande wa ufuatiliaji maendeleo ya kitaaluma na nidhamu kwa watoto wao, badala yake wamekuwa wakiwaachia walimu pekee mzigo mkubwa wa kuwalea watoto hao.

No comments: