Saturday, October 24, 2015

ASKARI MAGEREZA WAFARIKI BAADA YA KUPATA AJALI



Na Kassian Nandindi,
Songea.

ASKARI wawili wa Jeshi la magereza, gereza la mifugo la Majimaji lililopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wanasafiria kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela aliwataja askari hao waliopoteza maisha kuwa ni B 7303(Wader) Oscar Henry (29) na B 5361 CPL Geofrey Mwambigija (26) wote ni askari wa gereza hilo.

Alisema siku hiyo ya tukio, kwenye barabara inayotoka Tunduru kwenda Masasi pikipiki isiyofahamika namba za usajili ambayo ilikuwa ikiendeshwa na B 7303(Wader) Oscar Henry ikiwa kwenye mwendo kasi ilianguka na kusababisha vifo vyao.


Askari hao wawili walifariki dunia, mara baada ya kufikishwa hospitali ya wilaya Tunduru na kwamba pikipiki yao baada ya kupata ajali iliibiwa na watu wasiofahamika, ambao walikimbia na kutokomea nayo kusikojulikana.

Pamoja na mambo mengine, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa pikipiki hiyo ambayo ilimfanya ashindwe kumudu usukani na kwa hivi sasa Polisi, inaendelea kuwasaka watu walioiba pikipiki hiyo.

No comments: