Sunday, October 4, 2015

UHAMIAJI RUVUMA WATOA ONYO

Na Mwandishi wetu,
Songea.

IDARA ya uhamiaji   mkoa wa Ruvuma, imewaonya watu wasiokuwa raia wa Tanzania kutojihusisha kwa namna yoyote ile katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na endapo watafanya hivyo watakuwa wamekiuka sheria za nchi.

Mbali na hilo imeelezwa kuwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa mtu asiyekuwa raia wa Tanzania, kunaweza kusababisha taifa kupata viongozi wabovu wasiokuwa na uchungu wa kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Ofisa uhamiaji wa mkoa huo, Hilgaty Shauri alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mjini songea.


Shauri aliwataka wananchi hasa kwa wale wanaoishi maeneo ya mipakani, kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maafisa uhamiaji waliopo kwenye maeneo hayo, ili kudhibiti wahamiaji haramu  wanaoweza kuingia hapa nchini, na kushiriki katika zoezi la uchaguzi huo siku ya upigaji kura.

Alibainisha kuwa vita dhidi ya wahamiaji haramu, isiachwe ikafanywa na idara ya uhamiaji pekee, bali kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu ambapo watu hao watakapoingia hapa nchini licha ya kufanya shughuli ambazo Watanzania wenyewe wanaweza kuzifanya, lakini serikali italazimika kuwahudumia kwa kuamini kwamba ni raia wake hivyo kuibebesha mzigo mkubwa usiokuwa wa lazima.


Kutokana na hali hiyo, amewaomba pia Wenyeviti na Watendaji wa vijiji na  kata kuwa na utaratibu wa kukagua maeneo yao, hatua itakayosaidia kutambua watu wao na kuwabaini watu wanaoingia kinyume cha utaratibu za nchi.

No comments: