Thursday, October 15, 2015

WATAKIWA KUTUNZA SHAHADA ZAO ZA KUPIGIA KURA

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MGOMBEA nafasi ya ubunge Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhandisi Edwin Ngonyani, amewakumbusha wananchi wa jimbo hilo, kutunza shahada zao za kupigia kura na kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Aidha amewataka kuwakataa wagombea wanaotumia kiasi kikubwa cha fedha kuwahonga wapiga kura, ili waweze kuwachagua katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Ngonyani alisema kitendo hicho ni cha aibu na fedheha, hivyo kiongozi anayepatikana kwa mfumo huo akishachaguliwa hushindwa kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi wake, badala yake hutumia nafasi yake aliyonayo kuliingiza Taifa kwenye matatizo makubwa na kuwafanya wananchi anaowaongoza kuwa maskini.


Hayo yalisemwa na mgombea huyo, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Utwango kata ya Namabengo wilayani humo katika mkutano wake wa kampeni huku akisisitiza kwa kuwataka wananchi kuendelea na utamaduni wa kuheshimiana, kupendana na kuacha kubaguana kwa misingi ya itikadi ya dini au siasa.


Ngonyani alisema kwamba, iwapo atachaguliwa  kuwa mbunge wa Namtumbo atatumia uwezo na elimu aliyonayo kuhakikisha mgodi wa madini ya Uranium uliopo  mto Mkuju  katika pori la Selou, unasaidia kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana na wanawake wa wilaya hiyo, badala ya kuwanufaisha watu kutoka maeneo mengine.

No comments: