Tuesday, October 27, 2015

TUNDURU SONGEA CCM YAZIDI KUNG'ANG'ANIA MAJIMBO YAKE



Na Steven Augustino,
Ruvuma.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Tunduru na Songea mkoani Ruvuma, kimeendelea kung’ang’ania majimbo yake na kata kwa ujumla baada ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi.

Wakitangaza kwa nyakati tofauti wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya Tunduru Kusini, Kaskazini na Songea walisema kuwa wagombea wa chama hicho ndio walioibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Wilayani Tunduru msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo aliwatangaza Daimu Mpakate kupitia Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi wa nafasi ya ubunge, jimbo la Tunduru Kusini baada ya kupata kura 27,486.


Alisema katika matokeo hayo, Mpakate aliwashinda wapinzani wake Sadick Songoni wa Chama Cha Wananchi (CUF) kupitia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) aliyepata kura 16, 620 na Ally Abdallah, ACT Wazalendo aliyepata kura 1,026.

Kwa upande wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Sekambo alimtangaza Mhandisi Ramo Makani (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 29,841 na kuwashinda Manjoro Kambili (CUF) aliyepata kura 29,102 na Mohammed Alifa, ACT wazalendo aliyepata kura 856.

Katika jimbo la Songea mjini msimamizi wa uchaguzi, Lahari Kimari alimtangaza Leonidas Gama (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 40,886 na kuwashinda Fuime Joseph (CHADEMA) aliyepata kura 37,012 na kwamba upande wa matokeo ya udiwani Chama Cha Mapinduzi, kimeibuka na ushindi katika kata 16 kati ya 21 zilizopo kwenye jimbo hilo ambapo kata 5 zimechukuliwa na vyama vya upinzani.

No comments: