Saturday, October 24, 2015

WATAWANYWA KWA MABOMU YA MACHOZI BAADA YA KULETA VURUGU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KUNDI la watu linalodaiwa kuwa ni la wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limevamia eneo la soko la wakulima lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, na kung’oa kisha kuchana bendera 50 za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye thamani ya shilingi 200,000 kutokana na chuki za kisiasa zilizopo wilayani humo.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya asubuhi huko wilayani Mbinga.

Alifafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio, kundi hilo lilikwenda kwenye eneo hilo na kufanya vurugu kisha kungo’a milingoti iliyowekwa bendera na kuzichana jambo ambalo lilisababisha kuwepo kwa vurugu kubwa kati ya wafuasi wa CHADEMA na wa CCM.

  
Alisema kuwa wakati vurugu hizo zinaendelea, taarifa za tukio hilo zilikuwa tayari zimeshafika kwenye Kituo kikuu cha Polisi Mbinga na ndipo askari walijipanga na kwenda kwenye eneo la  tukio, ambako walifanikiwa kuwatawanya watu waliokuwa wakileta vurugu.

Kadhalika baadaye Polisi walilazimika kutumia mabomu kwa lengo la kuwatawanya watu hao waliokuwa wanaleta vurugu, ambapo hakuna madhara yoyote yaliyotokea.

Hata hivyo Polisi walifanikiwa kuwakamata watu watatu, ambao ndio inadaiwa walikuwa vinara wa kuanzisha vurugu hizo ambapo aliwataja kuwa ni Meshack Komba (26) mkazi wa Matarawe Mbinga mjini, Michael Ndimbo (20) ambaye ni dereva wa boda boda na Bushiri Mterera (30) wote wakazi wa Furaha Store.

Kamanda Msikhela alisema kuwa hivi sasa, jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kuwasaka wafuasi wengine wa CHADEMA ambao inadaiwa walishiriki kufanya uhalifu kwenye eneo la soko la wakulima, na kusababisha kutokea kwa hasara.

No comments: