Tuesday, October 20, 2015

WAUGUZI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YAO



Na Muhidin Amri,
Songea.

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, Sixbert Kaijage amewataka Wauguzi wanaofanya kazi ndani ya halmashauri hiyo kujituma na  kutekeleza majukumu ya kazi zao ipasavyo, ili waweze kuboresha huduma husika kwa jamii, jambo ambalo litawafanya waweze kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia wilaya hiyo, kusonga mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi, na wananchi kufanya shughuli zao wakiwa na afya nzuri.

Kaijage alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika kijiji cha Lundusi, mji mdogo wa Peramiho, wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Maposeni wilayani humo kuhusiana na  serikali ilivyojipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali,  za kiutendaji kwa watumishi wa halmashauri hiyo.


Alisema halmashauri yake inatambua kuwa  wauguzi wanakabiliwa na changamoto  mbalimbali, baada ya watumishi hao kuhamia katika mji huo kutokana na kukosekana kwa vituo vingi vya kutolea huduma ya afya na nyumba za kuishi,  hata hivyo wamejipanga kukabiliana na tatizo hilo  kwa kufanya ujenzi na kuongeza bajeti ambayo itawezesha kununua dawa na vifaa.

Mbali na hilo Kaijage alisema, serikali inatambua changamoto hizo hivyo itaendelea kuyashughulikia na kuyapatia ufumbuzi ili kuleta hamasa ya utendaji wa kazi kwa watumishi hao.

Aliongeza kuwa, mkakati wa kwanza wataimarisha miundombinu ya maji, barabara pamoja na umeme katika halmashauri ya Songea vijijini, ili watumishi waweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kupenda kuishi katika mji huo wa Peramiho.

Kutokana na hilo alisema, tayari wamempata mkandarasi  ambaye ataanza kujenga barabara za mji huo kwa kiwango cha lami  ambapo awali wataanza ujenzi wa kilometa saba, itakayoanzia makutano ya Ofisi za halmashauri hadi  hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho na nyingine itakayoelekea chuo cha madakatari, kilichopo katika kijiji cha Morogoro wilayani humo.

No comments: