Monday, October 26, 2015

MANYANYA AIBUKA KIDEDEA JIMBO LA NYASA

Injinia Stella Manyanya

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

TAARIFA zilizotufikia hivi punde Jimbo la Nyasa lililopo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuongoza na kupeperusha bendera yake kwa nafasi ya kiti cha udiwani, ubunge na rais dhidi ya vyama vya upinzani.

Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Jabir Shekimweri amezungumza na mwandishi wa habari hizi na kueleza kwamba kwa nafasi ya udiwani, mpaka sasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweza kuchukua kata mbili kati ya 18 zilizopo wilayani humo na matokeo kwa ngazi hiyo ya udiwani, bado yanapokelewa kutoka katika kata mbalimbali.

Alisema jimbo la Nyasa lina idadi ya wapiga kura 70,766 na kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 45,838.


Kwa nafasi ya ubunge, amemtangaza Injinia Stella Manyanya kupitia tiketi ya CCM kuwa mshindi nafasi ya ubunge ambaye amepata kura 31,548.

Shekimweri alisema kuwa CHADEMA kimepata kura 12,653 kwa nafasi hiyo ya ubunge ambapo kilimsimamisha mgombea wake, Ngwata Saulo na ACT Wazalendo kilimsimamisha, Raymond Ndomba aliyepata kura 497.

Kwa nafasi ya mgombea urais uchunguzi wetu umebaini kuwa jimbo la Nyasa, Chama Cha Mapinduzi kimejizolea kura nyingi na kufanya hata baadhi ya maeneo mbalimbali jimboni humo wapiga kura wakiwa wanasherehekea juu ya ushindi huo.

Nafasi ya rais Mkurugenzi huyo amesema yeye hana mamlaka ya kutangaza badala yake, wanayapeleka katika ngazi husika ili yaweze kutangazwa.

Pamoja na mambo mengine, licha ya wilaya ya Nyasa kukabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara wasimamizi wa uchaguzi wameweza kuwasilisha matokeo husika, huku ya ngazi ya udiwani yakiwa bado yanaendelea kukusanywa kutoka katika kila kata na kwamba uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu hakuna dosari yoyote iliyojitokeza.

No comments: