Monday, October 12, 2015

MAMBO MAZURI TUNDURU WAIBUKA KIDEDEA

Na Steven  Augustino,
Tunduru.

TIMU ya soka, Mambo Mazuri FC ya Tunduru mjini mkoani Ruvuma, imeibuka kidedea kupitia ligi ya Polisi Jamii, baada ya kuwafunga  mahasimu wao, Vampire FC magoli manne kwa matatu katika mchezo mkali, uliorindima kwenye uwanja wa Chama Cha Mapinduzi mjini hapa.

Kutokana na matokeo hayo, Vampire FC imeambulia nafasi ya pili na mshindi wa tatu katika mashindano hayo ikachukuliwa na Jobe FC.

Kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Mratibu wa mashindano hayo,  Inspector Songelael Jwagu mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atazawadiwa kikombe, seti moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu.


Inspector Jwagu alifafanua kuwa, mshindi wa pili atapata zawadi ya seti moja ya jezi na wa tatu atajinyakulia mpira mmoja wa miguu.

Alisema jumla ya timu 12 zilishiriki katika mashindano hayo, ambapo kati yake timu 16 zilitolewa katika ligi ya mtoano iliyochezwa na kubakia timu nane.

Kadhalika alizitaja timu  zilizoendelea na ligi hiyo katika mzunguko wa pili kuwa ni Joker FC, Tunduru Seko Fc, Usalama FC, Mambo mazuri FC, Veterani FC, Jobe FC, Tunduru City na Vampire FC.

Aidha katika taarifa hiyo pia alizitaja timu zilizoshiriki na kutolewa katika mzunguko wa kwanza kuwa Frank FC, Red Scud FC, Nakayaya FC,  Mgomba FC, River Kombaini FC, Fridom FC na Joker FC.

Wakati wa makabidhiano ya zawadi hizo kwa washindi hao, Kamanda wa Polisi wilayani Tunduru, Nicholaus Mwakasanga alisema pamoja na mashindano hayo kutoa ujumbe wa Polisi jamii na kuwataka wananchi kushiriki katika mpango wa ulinzi shirkishi, pia alizitaka timu hizo kucheza michezo ya kupendana, kushirikiana kwa kile alichoeleza kuwa michezo ni furaha.


Kamanda Mwakasanga aliwataka vijana kuachana na vitendo vya matumizi ya madawa ya kulevya, kufanya matukio ya uhalifu na kukataa kutumiwa na wanasiasa ambao wamekuwa wakiwashawishi na kuwatumia vibaya katika kufanya maandamano, bila kufahamu chanzo chake hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

No comments: