Wednesday, October 21, 2015

ASKARI WAASWA KUTOTUMIA NGUVU WAKATI WA UCHAGUZI

Na Steven Augustino,

Tunduru.

ASKARI ambao watashiriki katika jukumu la kulinda amani na utulivu, siku utakapofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, wametakiwa kupunguza matumizi ya nguvu zisizokuwa za lazima katika uchaguzi huo.

Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Nicolaus Mwakasanga alisema hayo alipokuwa akifungua juzi mafunzo elekezi yaliyoshirikisha askari polisi, magereza, uhamiaji na mgambo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.

Mwakasanga alisema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuweza kufanikisha na kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unakwenda salama.


"Sisi ni walinzi, inatupasa tuwe wavumilivu na wastahimilivu wakati wa kutekeleza majukumu yetu, tuache kutumia nguvu kubwa pale ambapo hakuna sababu ya msingi", alisisitiza Mwakasanga.

Alisema katika kikao hicho askari hao, watapewa maelekezo muhimu watakayotakiwa kuyafuata wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika.

Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa baadhi ya mambo muhimu watakayotakiwa kuyafuata katika utekekelzaji wa zoezi hilo kwamba, askari hao watajengewa uwezo katika masuala ya usimamizi wa haki za binadamu, utatuzi wa migogoro kabla haijatokea, masuala ya jinsia na utekelezaji wa majukumu yao wakati wa uchaguzi.

Wakifafanua kwa nyakati tofauti wakufunzi wa mafunzo hayo, Inspekta Joseph Malongo na Anosisye Mwaipopo walisema kuwa asilimia 90 ya utekelezaji wa majukumu ya Polisi, wengi wao hufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu hivyo aliwataka kuachana na vitendo hivyo na kuzingatia sheria husika na sio vinginevyo.

No comments: