Friday, October 2, 2015

MGOMBEA UBUNGE MHANDISI RAMO MAKANI AANGUKA JUKWAANI

Mhandisi Ramo Makani akiwa amedondoka katika jukwaa la mkutano, wakati alipojaribu kuiga staili ya mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli ya kupiga "Push up".

Mhandisi Ramo Makani, akiinuliwa na walinzi wake. (Picha zote na Steven Augustino)
Na Steven Augustino,
Tunduru.

MGOMBEA ubunge Jimbo la Tunduru kaskazini, Mhandisi Ramo Makani kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameanguka jukwaani, wakati alipokuwa amekwisha panda kwenye jukwaa hilo, akijiandaa kuomba kura kutoka kwa wananchi.

Tukio hilo ambalo lilionekana kuwashangaza watu wengi, waliokuwa wamekusanyika kwenye mkutano wake wa kampeni katika viwanja vya Baraza la Idd mjini hapa, ambapo Ramo alikumbwa na mkasa huo wakati alipokuwa akijaribu kuiga staili ya mgombea Urais, John magufuli ya kupiga “push up” kabla ya kuanza kunadi sera zake.

Ingawa tukio hilo lilionekana kumtia aibu, huku baadhi ya wanachama wake wakizomea na wengine kucheka lakini alijikakamua kuinuka, huku akisaidiwa na walinzi wake waliokuwa karibu naye.


Kufuatia hali hiyo mgombea huyo wa CCM, alishindwa kunadi sera za chama chake na kulazimika kuwaeleza maelfu ya wananchi waliokuwa wamekusanyika kwenye mkutano huo kwa ajili ya kumsikiliza, kwenda kusoma vitabu alivyodai kuandika mambo yote aliyoyafanya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Katika kipindi kilichopita, nimetekeleza ilani ya chama changu kwa kusimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo hadi Tunduru, na wilaya ya Nanyumbu ambayo sasa inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami pia kuna mradi wa umeme vijijini hapa wilayani ambao unaendelea kujengwa”, alisema Mhandisi Ramo.

Sambamba na kuwepo kwa taharuki hiyo, kadhalika mgombea huyo aliwaeleza wananchi kwamba wajiandae kupokea mabadiliko kauli ambayo iliwafanya wengi wao wanaounga mkono, vyama vinavyounda UKAWA kushangilia kwa nguvu huku wakizungusha mikono yao kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika mikutano yao ya kampeni ya vyama hivyo.


Awali katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Tunduru, Hamis Kaesa naye alionekana kutoendana na malengo ya mkutano huo baada ya kuhoji umati huo kwamba ni nani hatompigia kura Mhandisi Ramo, jambo ambalo liliwafanya watu wasiompenda mgombea huyo kuinua mikono yao juu bila uoga.

No comments: