Tuesday, October 13, 2015

TASAF NAMTUMBO YASEMA BAADHI YA WANASIASA WANAPOTOSHA WANANCHI

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

OFISA ushauri na ufuatiliaji, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hapa nchini wilaya ya  Namtumbo   mkoani Ruvuma,  Edson  Kagaruki  amekanusha  taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wilayani humo, kwamba mfuko huo unafanya kazi ya kuhawilisha fedha kwenda kaya maskini, kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika, Oktoba 25 mwaka huu.

Kufuatia maneno hayo, Ofisa huyo wa TASAF  wilayani humo amewataka wanasiasa hao kuacha porojo  hizo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali, katika kupambana na umaskini hapa nchini.

Aidha amewakumbusha kutumia majukwaa ya kisiasa, kueleza sera zao na sio kuwapotosha wananchi kwa mambo ambayo hayana msingi, jambo ambalo linaweza kuchochea uhasama katika jamii.


Kagaruki alisema kuwa amechukua jukumu la kutoa ufafanuzi huo, baada ya kuwepo kauli  kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wilayani Namtumbo wanaodai kuwa, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) ni njama na ujanja wa Chama cha Mapinduzi kutaka kujiweka karibu na wapiga kura, ili wakichague katika uchaguzi huo.

Alifafanua kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, kwani mpango huo unalenga kunusuru kaya maskini na tokea uanzishwe hapa Tanzania una zaidi ya miaka mitatu, na baadhi ya wananchi kupitia Halmashauri husika wamewezeshwa kupitia mpango huo.

Kwa mujibu wa Kagaruki alieleza kuwa TASAF, ilianza kazi zake siku nyingi katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika awamu tatu na haina uhusiano wowote na chama cha siasa, zaidi ya kuboresha maisha ya Watanzania waliowengi ambao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali.

Alifafanua kuwa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, ina vijiji 42 ambavyo vipo kwenye mpango wa uhawilishaji fedha na tayari malipo ya awamu ya pili yameshafanyika, Septemba 28 mwaka huu.

Mbali na hilo, alisema katika vijiji hivyo jumla ya kaya 5,652 ambazo zilikidhi vigezo na kuingizwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini, vilipewa fedha ambazo zitawawezesha kupunguza ukali wa maisha katika familia zao.

Alisema kuwa Halmashauri hiyo, itatumia kiasi  cha shilingi milioni 237,577,500.00  ili kufanikisha zoezi zima, la malipo kwa walengwa.

Kwa upande wake  Mratibu wa TASAF wilaya ya Namtumbo,  Raphael Mponda alisema kupitia mpango huo walengwa, hupata ruzuku ya msingi  na wengine ya kutimiza masharti.

Alifafanua kuwa ili kaya yenye watoto iweze kupata ruzuku, lazima watoto waliochini ya miaka mitano wapelekwe Kliniki na kupata huduma za afya kwa asilimia mia moja, na wale walio na umri wa kwenda shule wanatakiwa kuhudhuria masomo yao kwa kiwango kisichopungua asilimia 80 ya siku zote za masomo.


Fedha hizo za malipo kwa kaya masikini, hufanyika kila baada ya miezi miwili na kwamba matumaini yake kupitia mpango huo walengwa wataweza kuboresha maisha yao, kuweka akiba na kuanzisha shughuli mbalimbali za kuinua uchumi katika kaya zao.

No comments: