Friday, April 19, 2013

TUNDURU SEKTA YA ELIMU BADO NI TATIZO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEBAINISHWA kuwa mahusiano mabaya kati ya Walimu na Wanafunzi ni moja kati ya kikwazo kilichoelezwa kwamba huchangia kuzorota kwa elimu wilayani humo.

Kadhalika  wanafunzi kukataa kukaa katika mabweni au hosteli ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo ya elimu wilayani Tunduru na kusababisha wilaya hiyo kupata matokeo mabaya kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha pili na nne katika kipindi cha mwaka 2011/2012.

Hayo yalibainishwa na afisa elimu sekondari Ally Mtamila wakati akiwasilisha taarifa yake ya matokeo ya kidato cha pili na cha nne katika kipindi cha mwaka 2011/2012 katika mkutano maalum ulioketi wilayani humo, na kuongeza kwa kuwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika usimamiaji wa watoto wao ili waweze kuwa na hamasa ya kupenda masomo wanapokuwa shuleni au nyumbani.

Monday, April 15, 2013

BREAKING NEWS: MVUA YASABABISHA MAAFA WILAYANI NYASA, MAKAZI YA JAA MAJI, MTU MMOJA AFARIKI DUNIA NA EKARI 45 ZA SOMBWA NA MAJI

Ziwa Nyasa.


















Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

YAMEJITOKEZA maafa makubwa  wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha wilayani humo, na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia, mazao yaliyolimwa shambani na mifugo kusombwa na maji.

Tukio hilo limetokea usiku wa tarehe 14 mwaka huu, ambapo watu wamekosa mahali pa kuishi kutokana na nyumba zao kujaa maji na kulazimika, kwenda kuomba msaada kwa majirani wenzao.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa wilaya hiyo Ernest Kahindi alisema kunyesha kwa mvua hizo kumesababisha kuwepo kwa maji mengi yaliyokuwa yakitokea milimani na kuelekea kwenye makazi ya watu.

Friday, April 12, 2013

MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA ZA ASILI YATABORESHA ZAO LA KAHAWA


Upande wa kushoto mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd wa kampuni ya Sustainable Harvest, ya kutoka wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, akiwa katika eneo la shamba darasa la kilimo cha kahawa, kikundi cha Unango kata ya Ngima wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, akiwaelimisha wakulima wa zao hilo kuzingatia kanuni za kilimo bora.(Picha na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,



KAHAWA ni moja kati ya bidhaa muhimu na maarufu inayopendwa duniani, vilevile ni chanzo cha mapato kwa nchi zinazozalisha zao hilo.
     
Uzalishaji wa zao hili si kazi rahisi bali ni kazi ngumu inayohitaji ujuzi wa hali ya juu, na kwamba  ili kuwawezesha wakulima kuzalisha zao hilo kwa viwango vyenye ubora, mara zote sekta husika zimekuwa zikiwaelimisha wakulima hao mara kwa mara namna ya uzalishaji huo.

Tanzania ni moja kati ya nchi inayozalisha kahawa, huku jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa ili kuboresha uzalishaji wake kwa ushirikiano, kati ya serikali na taasisi binafsi.

BREAKING NEWS: WAANDISHI WAWILI NA AFISA UHAMIAJI WAFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI MKOANI TANGA

IGP Said Mwema























Na Mwandishi wetu,
Tanga.

AJALI mbaya iliyotokea jana wilaya ya Handeni mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu watatu, ambao ni waandishi wa habari wawili kutoka kampuni ya Mwananchi Communication na gazeti la Uhuru na Mzalendo, Radio Aboud na Ofisa Uhamiaji wa wilaya hiyo.
 
Ajali hiyo iliyotokea Aprili 11 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi iliuhusisha msafara wa Mkuu wa wilaya hiyo Muhingo Rweyemamu, ni msafara unaodaiwa kuwa ulikuwa na magari matatu tu lakini gari moja liliacha njia na kupinduka.

Waliofariki ni pamoja na Hussein Semdoe mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Hamis Bwanga wa Radio Uhuru na Abood pamoja na Mariam Hassan ambaye ni Ofisa Uhamiaji wilaya ya Handeni.

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo pamoja na vifo vya marehemu hao.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Mkuu wa wilaya hiyo alisema ajali hiyo ilitokea wakiwa kwenye msafara, kuelekea Ndolwa kupanda miti.

Muhingo alieleza kwamba gari lililopata ajali ni la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni, lenye namba za usajili STJ 4673 ambalo ndilo lililokuwa likitumiwa na Ofisa Uhamiaji, Hassan pamoja na wanahabari hao.

Alisema huu ni msiba  mkubwa kwa wilaya ya Handeni kwani wamepoteza wachapakazi na watu muhimu katika mchakato wa maendeleo ya wilaya hiyo.

"Wilaya ya Handeni imepoteza wanahabari kwa asilimia 100, kwani waandishi hawa ndiyo walikuwa wanahabari pekee wilayani hapa,

"Msiba huu ni mkubwa si kwa tasnia ya wanahabari pekee bali hata kwa juhudi za maendeleo ya wilaya ya Handeni, tulikuwa tukizunguka nao katika shughuli mbalimbali hapa wilayani hivyo ni pigo kubwa," alisema Muhingo.
 
Aidha Mkuu wa wilaya hiyo alisema marehemu Hassan ambaye alikuwa afisa uhamiaji kabla ya umauti alikuwa mpambanaji mkubwa wa wahamiaji haramu katika wilaya hiyo.

Aliongeza kuwa hivi karibuni alifanikiwa kuwakamata takribani wahamiaji 70 eneo hilo, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa nguvu kazi ya wilaya ya Handeni.

Miili ya waandishi imechukuliwa na ndugu na kwamba serikali inatoa pole kwa ndugu na jamaa waliopatwa na matatizo hayo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga Costantine Massawe amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.

Thursday, April 11, 2013

BREAKING NEWS: MWANDISHI NA OFISA UHAMIAJI WAFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI, WENGINE WAJERUHIWA VIBAYA



Na Mwandishi wetu,
Tanga.

WATU wawili wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa vibaya hivi punde, baada ya kutokea ajali katika wilaya ya Handeni wilayani Tanga.

Waliofariki dunia ni Mwandishi wa habari wa Uhuru na Mzalendo na Radio Aboud, Hamis Bwanga na Ofisa uhamiaji wa wilaya ya Handeni, Mariam Hassan akiwemo pia Mwandishi wa gazeti la Mwananchi Hussein Semdoe ambaye amejeruhiwa vibaya na hali yake sio nzuri mpaka sasa.

VIKONGWE WAKAMATWA WAKIWAFUNDISHA WATOTO USHIRIKINA, WASWEKA RUMANDE KULINDA USALAMA WAO

Na Steven Augustino,

Tunduru.

VIKONGWE wa tano kutoka katika kijiji cha Mtonya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamezuiliwa katika kituo kidogo cha polisi Nakapanya, ili kulinda usalama wa maisha yao na kuwafanya wasishambuliwe kutokana na kutuhumiwa kufanya ushirikina na kuwafundisha taaluma hiyo watoto wa watu bila ridhaa ya wazazi wao.

Tukio hilo lilitokea baada ya vikongwe hao wanaodaiwa kuwa na uwezo wa kufungua na kuingia katika nyumba za watu kwa njia za kishirikina, walifumwa wakifanya vitendo hivyo katika kijiji cha Mindu wilayani humo.

Taarifa zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nakapanya Kubodola Ambali, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Spia Msusa (50), Ayana Iddi (75) Adresia Maulid (68), Jenifer Saimon(60) na mwingine aliyefahamika kwa jina la Biti Nyoya mwenye umri wa miaka 60.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUVAMIWA NA TEMBO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Daraja mbili kata ya Namwinyu tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Chalamanda  Masapi (65) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na Tembo.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa marehemu Masapi  alikumbwa na mkasa huo  baada ya kukutana na tembo huyo ambaye alikuwa na mtoto, ghafla wakati akikagua uharibifu wa mazao uliofanywa na kundi la wanyama hao, katika shamba lake lililopo nje kidogo na kijiji hicho.

Mtoto wa marehemu Chalamanda ambaye alikuwa ni miongoni mwa shuhuda wa tukio hilo Rashid Chalamanda  alisema, yeye na marehemu baba yake kwakushirikiana na kundi la wananchi wanaolima katika eneo hilo, walikwenda katika mashamba yao kushiriki katika zoezi la kuwafukuza tembo hao ambao pia walivamia kijijini hapo na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao yao.

Tuesday, April 9, 2013

UHURU AAPISHWA KUWA RAIS WA KENYA, AHUTUBIA TAIFA

Kulia ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Wiliiam Ruto baada ya kuapishwa hivi punde.



















UHURU Kenyatta ameapishwa kuwa rais mpya wa Kenya akifuatiwa na William Ruto ambaye hivi punde ameapishwa naye kuwa Makamu wa Rais wa Kenya.

Msajili wa Mahakama, Gladys Shollei ndio amemuapisha Uhuru Kenyatta kuwa rais wa nne Kenya na baadaye amemuapisha William Ruto kuwa Makamu wa Rais wan chi hiyo.

Marais mbalimbali wamewasili  hivi punde katika Uwanja wa Karasani kwa ajili ya kushudia kuapishwa kwa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AOMBWA KUINGILIA KATI SUALA LA KUINUA KIWANGO CHA MPIRA WA MIGUU NA MIKONO MBINGA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.




















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WADAU wa michezo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamemuomba Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga, kuingilia kati suala la kuinua kiwango cha mpira wa miguu na mikono wilayani humo.

Vilevile wadau hao walisema endapo mkuu huyo wa wilaya atafanya hivyo, wana hakika kiwango cha mpira wilayani humo kitaenda vizuri, na kuifanya wilaya hiyo wananchi wake waweze kupenda michezo.

Hayo yalisemwa na wadau hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu, kwa nyakati tofauti mjini hapa.

Wednesday, April 3, 2013

TUNDURU WALIA NA HALI NGUMU YA MAISHA, KUTOKANA NA WAJANJA WACHACHE KUJINUFAISHA KATIKA ZAO LA KOROSHO



Na Steven Augustino,

Tunduru.


CHAMA cha Wananchi CUF Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kimewaomba wananchi wa wilaya hiyo kutotoa nafasi kwa viongozi watakaosimamishwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo.

Hayo yalibainishwa na Viongozi wa chama hicho wakati wakizungumza katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika viwanja vya baraza la Idd na kuongeza kuwa kauli hiyo wanaitoa kufuatia viongozi wa CCM waliopewa dhamana na wananchi kushindwa kutimiza wajibu wao.

Mkurugenzi wa haki za bianadamu na sheria  Mtukumbe Selemen Issa Ismail na Katibu wa CUF wilaya  Mchemela Salum Abudalah  ni miongoni mwa waliobainisha maelezo hayo, na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na viongozi waliopewa mamlaka hayo kutotimiza wajibu wao na kusababisha hata zao la Korosho wilayani humo, wakulima kukosa soko la uhakika.

KITUO CHA KULELEA WATOTO YATIMA TUNDURU, WAOMBA MSAADA



Na Steven Augustino,

Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imeahidi kutoa msaada wa shilingi milioni 2.8 katika kituo cha kulelea watoto yatima, kinachomilikiwa na Kanisa la Bibilia kijiji cha Mbesa  wilayani humo ikiwa ni juhudi yake ya kujali watoto hao.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Nehatta wakati akizungumza kwenye  maadhimisho ya Wanawake wa kikristo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.

Tayari fedha hizo zimekwisha pewa Baraka na Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo na kupitishwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014.

Monday, April 1, 2013

UZINDUZI WA ALBAMU YA INJILI WAFANA, MKUU WA WILAYA YA MBINGA AWATAKA WANANCHI KUJENGA USHIRIKIANO

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga (Aliyeinama katikati) akiingiza DVD yenye nyimbo za Injili zilizotungwa na Rose Mahenge kwenye radio, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa albamu ya Waweza zeeka mapema, uliofanyika kwenye ukumbi wa Uvikambi mjini Mbinga. (Picha na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano na sio kujengeana ubaguzi, ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kusukuma mbele gurudumu la kimaendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Sambamba na hilo wametakiwa kushiriki kikamilifu katika suala zima la ulinzi na usalama, ili wilaya hiyo iweze kuwa na amani na utulivu na hatimaye wananchi wilayani humo, waweze kuishi kwa raha mustarehe bila kuwepo vikwazo vya hapa na pale.

Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa albamu ya nyimbo za injili, ‘Waweza zeeka mapema’ iliyotungwa na mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili wilayani humo Rose Mahenge, uzinduzi ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo Mbinga mjini.

Wednesday, March 27, 2013

MWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI ROSE MAHENGE KUTUMBUIZA WANAMBINGA SIKU YA SHEREHE ZA PASAKA


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MWIMBAJI wa muziki wa Injili kutoka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Rose Mahenge anatarajia kufanya uzinduzi wa albamu mpya iitwayo Waweza zeeka mapema, siku ya sikukuu ya Pasaka Machi 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Uvikambi uliopo Mbinga mjini.

Akizungumza na Mtandao huu Mahenge anasema uzinduzi huo utashirikisha wasanii maarufu nchini, Senga na Pembe kutoka Jijini Dar es salaam ambao nao watakuwa wakitumbuiza na kutoa burudani za aina mbalimbali siku hiyo.

AKINA MAMA TUNDURU WALIA NA HUDUMA ZA AFYA


Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI imekumbushwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, ili kuondoa kero ambazo zimekuwa zikilikabili kundi la wanawake na akina mama wajawazito, pale wanapohitaji kupatiwa huduma za matibabu na wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na baadhi ya wanawake walioshiriki katika vikundi vya kwaya, ngoma, maigizo na ngonjera zilizofanyika wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mchoteka wilayani Tunduru hapa mkoani Ruvuma.

MKUU WA WILAYA ALIA NA WANAOKWAMISHA MRADI WA USHOROBA, JESHI LA POLISI LAAGIZWA KUWACHUKULIA HATUA WAHUSIKA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JESHI la polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeagizwa kuhakikisha kwamba linafanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu walioshiriki katika zoezi la hujuma za kubomoa jengo la mradi wa Ushoroba na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 36.9.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alitoa agizo hilo katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama, kilichoketi kwa ajili ya kujadili hasara za uharibifu wa mradi huo, ambao unajengwa kijiji cha Lukala kilichopo Kata ya Mchesi tarafa ya Lukumbule wilayani humo.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na nchi ya Ujerumani, unajengwa ikiwa ni juhudi ya mwendelezo mradi wa ushirikiano wa kudhibiti vitendo vya ujangili, ambao umekuwa ukifanywa na wawindaji haramu katika nchi za Tanzania na Msumbiji.

WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE TUNDURU KUBURUTWA MAHAKAMANI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JUMLA ya kesi 1064 zinazowahusu wazazi na walezi walioshindwa kupeleka watoto wao shule, zimepangwa kuanza kusikilizwa ikiwa ni juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari, wanapelekwa shule.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alisema hayo huku akifafanua kuwa, kesi zote zimepangwa kufanyika katika vijiji husika vya wilaya hiyo.

Nalicho alisema hali hiyo imetokana na wazazi hao kuendelea kukaidi maelekezo ya kupeleka watoto wao shule, hali               iliyoisukuma serikali kumtafuta hakimu, ambaye atahamishia shughuli za mahakama vijijini, ili kurahisisha kazi za utekelezaji wa sheria.

WANANCHI WA KATA YA NAMASAKATA TUNDURU WALILIA MAJI, WASEMA WAPO TAYARI KUTOA MTU KAFARA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATA ya Namasakata wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,  wametishia kutoa kafara ya mtu achinjwe, kwa ajili ya tambiko litakalosadia wananchi wa kata hiyo, kupata huduma ya maji safi na salama.

Diwani wa kata hiyo Masache Ally alisema hayo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kufuatia adha kubwa wanayopata wananchi wake juu ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Alisema wamechoshwa na danadana na ahadi hewa zinazotolewa na serikali juu ya utekelezaji na utatuzi wa tatizo hilo.

Monday, March 25, 2013

MAKAA YA MAWE YAMPONZA GAUDENCE KAYOMBO, ATAMANI KUJIUZURU

Gaudence Kayombo Mbunge Mbinga Mashariki.


















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI siku zote wamekuwa wakiamini kwamba, kiongozi yeyote aliyewekwa madarakani, ni mtetezi na msimamizi mkuu wa maendeleo yao katika eneo husika.

Kana kwamba hilo halitoshi, baadhi yao wakishawekwa madarakani wanaonekana kuwa mwiba kwa wananchi, na hata kutotimiza ipasavyo majukumu yao ya kazi.

Jamii siku zote hufikia hatua ya kupoteza imani kwa viongozi wao endapo tu, pale wanapobaini msimamizi wao wa maendeleo tayari yupo katika mrengo wa kushoto dhidi yao, wakimuona akijijengea maslahi yake binafsi na kusahau wananchi anaowatumikia.

Tatizo hili likigundulika ndio maana utakuta migogoro au malalamiko ya hapa na pale huanza kujitokeza, na kiongozi husika kunyoshewa kidole wakati mwingine kusababisha kutokea kwa vurugu zinazoweza kuhatarisha amani katika eneo husika.

MALI ZA USHIRIKA MBICU UTATA MTUPU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga. 

KAMA serikali mkoani Ruvuma, haitachukua hatua za haraka katika kusimamia na kukabidhi kwa njia halali mali za chama cha ushirika MBICU kilichopo wilayani Mbinga mkoani hapa, hakika huenda wanachama wenye mali hizo wasinufaike nazo.

Kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta hapa wilayani, kutokana na viongozi husika kudaiwa kukabidhi mali za ushirika huo kwa njia za siri, bila wanachama ambao ni wakulima wa ushirika huo kupewa taarifa kamili juu ya hatma ya mali zao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kwamba, MBICU ni chama cha ushirika kinachojumuisha wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga.

MIRADI YA UMWAGILIAJI MBINGA MASWALI MENGI KULIKO MAJIBU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

ENDAPO Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, itaendelea kupuuzia na kufumba macho juu ya usimamiaji na ujenzi bora wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji, hakika maendeleo katika sekta ya kilimo hicho cha umwagiliaji hapa wilayani yataendelea kudorola.

Siku zote jamii imekuwa ikitambua kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote ile hapa duniani na ni tegemeo kwa wataalamu husika waliopo katika sekta hiyo, kuendeleza miradi mbalimbali ya kilimo hicho, ili wananchi wake hususani wakulima waweze kuzalisha mazao yao shambani kwa ubora unaokubalika.

Mwandishi wa makala haya anaelezea juu ya utata uliopo katika mradi wa umwagiliaji wa Sangamabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi, ambapo umekuwa ukizua malalalamiko kutoka kwa wananchi kwamba ujenzi wake unashindwa kuendelea kutokana na uongozi wa wilaya hiyo, kushindwa kusimamia kikamilifu na kufuata taratibu husika za wataalamu wa kanda ya umwagiliaji Mtwara.

WALIA NA MWEKEZAJI WA MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

TANZANIA  ni nchi ambayo imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika kwa ufasaha, taifa hili wananchi wake kwa asilimia kubwa wanaweza kuondokana na umasikini ambao umekuwa ukiitesa jamii nyingi miongoni mwao.

Lakini inashangaza kuona licha ya kuwa na rasilimali hizo kama vile madini ya aina mbalimbali, bado wananchi wake wamekuwa wakilalamika kila kukicha kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.

Malalamiko hayo yamekuwa yakielekezwa hasa kwa viongozi wa serikali ambao ndio wamepewa dhamana na kusimamia misingi na taratibu nzuri ambazo zitamfanya Mtanzania aweze kunufaika nazo.

Chakusikitisha baadhi ya viongozi wetu ambao ndio wamepewa jukumu hilo, wanaonekana kutozingatia taratibu husika, na kusababisha kelele na hata maandamano yasiyokuwa ya lazima ambayo yanafanywa na wananchi wa eneo fulani ambako kero husika inatokea, yakilenga kudai haki zao.

Friday, March 1, 2013

WAZEE WA TUNDURU WAIJIA JUU CCM


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la wazee wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limeazimia kufanya kikao cha dharula na kuiteua tume itakayo kwenda kuonana na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya kikwete na kupeleka kilio na kero za wananchi wa wilaya hiyo.

Wakifafanua taarifa hiyo kwa nyakati tofauti Mwenyekiti mstaafu wa CCM wilaya hiyo Kanduru Kassim,  na mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kapopo walisema kuwa hali
hiyo imetokana na kuwepo kwa tabia za viongozi wa chama na serikali wilayani humo, kupuuza kero na malalamiko ya wananchi wa wilaya hiyo.

Walisema licha ya malalamiko hayo ambayo yanafahamika, lakini chama na serikali vikiwa vimekaa kimya, hivyo baraza hilo limeadhimia kukutana na kuainisha kero zote na kuzianisha tayari kwa safari hiyo zikiwa ni juhudi za kukinusuru chama cha mapinduzi.

BWANA AFYA TUNDURU KUKIONA CHA MOTO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA cha Wanachi CUF kimetoa siku 14 kumtaka Bwana afya wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kutoa kibali cha kufungua Mbesa Hoteli iliyopo mjini humo, vinginevyo watafanya maandamano hadi katika ofisi za Mkuu wa wilaya hiyo kushinikiza hoteli hiyo ifunguliwe.

Tamko la kutaka kufanya maandamano hayo, lilitolewa katika mkutano wa kumkumbuka mwanzilishi na Mwalimu wa Siasa wilayani humo, marehemu Mazee Rajab aliyefariki Februari 17 mwaka 2010, uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru.


Lengo la kumtaka mkuu huyo wa wilaya Chande Nalicho kufungua hoteli hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa, hoteli hiyo iliyopo katika mji huo imefungwa kwa njia ya uonevu.

Thursday, February 28, 2013

POLISI RUVUMA YAFANIKIWA KUNASA SILAHA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kuzima tukio la ujambazi ambalo lilikuwa likifanywa katika mji wa Tunduru mkoni humo,  kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Deusdedit Nsemeki alisema kuwa taarifa za kukamatwa kwa bunduki hiyo yenye namba 5637002531 zilifanikiwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Alieleza kuwa bunduki hiyo bado haijajulikana inatoka nchi gani, na kwamba imepatikana baada ya polisi kupata taarifa za kiintelijensia, juu ya kuwepo mpango wa kufanyika tukio la ujambazi wilayani Tunduru.

Saturday, February 23, 2013

HAPPINESS KOMBA AKIPOKEA CHETI CHA KUHITIMU KIDATO CHA SITA KATIKA SHULE YA SEKONDARI AGUSTIVO ILIYOPO WILAYANI MBINGA

Mwanafunzi wa kidato cha sita Happiness Komba akipokea cheti cha kuhitimu kidato hicho katika mahafali ya tatu ya kuhitimu masomo yake, shule ya sekondari Agustivo iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Anayemkabidhi cheti hicho ni Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Mission Africa, Emmilian Kapinga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.(Picha na Julius Konala)

WANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA AGUSTIVO SEKONDARI WAKIFUATILIA KWA MAKINI MATUKIO MBALIMBALI YALIYOKUWA YAKIFANYIKA SIKU YA MAHAFALI YAO
















Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Agustivo iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, (waliovaa nguo nyekundu) wakiwa na wazazi wao wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi katika mahafali hayo Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Mission Africa, Emmilian Kapinga ambaye hayupo pichani, ambapo aliwaasa wazingatie masomo huko waendako.(Picha na Julius Konala)

WADAU WA ELIMU MBINGA WASHAURIWA KUJENGA MSHIKAMANO




Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Agustivo iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakitumbuiza katika mahafali ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo jana.(Picha na Kassian Nyandindi)





Na Julius Konala,
Mbinga.

WADAU wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujenga mshikamano katika kuendeleza na kukuza kiwango cha elimu wilayani humo.

Sambamba na hilo wametakiwa kujenga mshikamano katika kuhakikisha kwamba watoto wao, wanafuatilia kwa umakini masomo yao darasani.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Mission Africa, Emmilian Kapinga wakati akihutubia katika mahafali ya kidato cha sita shule ya sekondari Agustivo iliyopo mjini hapa.

Friday, February 22, 2013

KANISA LAPIGWA MOTO TENA ZANZIBAR, WALIANZA KULIPIGA MAWE, WAHUSIKA WASAKWA, UTARATIBU WA KUYALINDA NA POLISI WAANDALIWA

WATU wasiofahamika, wamelishambulia kwa mawe na kulichoma moto Kanisa la Walokole la Shaloom lililopo eneo la Kiyanga kwa Sheha, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
 

Tukio hilo limetokea juzi saa 9:30 usiku siku mbili tangu kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar, aliyepigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika.

Padri Mushi aliuawa wakati akishuka katika gari lake ili kwenda kuongoza ibada kwenye Kanisa la Betras ambapo wauaji hao, walikuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, ACP Augostine Olomi, alisema moto huo ulizuka kanisani hapo baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana wakipita karibu na kanisa hilo.

“Baada ya muda, mlinzi wa kanisa hili alisikia kishindo cha mawe juu ya paa hivyo alilazimika kukimbia na kwenda kujificha huku akiangalia kwa mbele kinachoendelea,” alisema Kamanda Olomi.

Aliongeza kuwa, wakati mlinzi huyo akiwa amejibanza mafichoni, aliona moto ukiwaka ndani ya kanisa ndipo alipopiga simu kwa kiongozi wa kanisa hilo ambaye naye aliwajulisha polisi.

Alisema baada ya polisi kufika eneo la tukio, walisaidiana na wananchi kuuzima moto huo ambao tayari ulishateketeza thamani za kanisa na vitu vingine vilivyokuwa ndani.

Kamanda Olomi alisema, moto huo ungeweza kusababisha athali kubwa kama usingedhibitiwa mapema ambapo dali zakeambazo ni Gibsam, zimesaidia kuunusuru moto huo usifike kwenye paa kuliteketeza kabisa.

“Wakati uongozi wa kanisa ukifanya tathmini ya hasara waliyoipata kutokana na moto huu, Jeshi la Polisi limeanza kuwasaka wahusika wa tukio hili kwa kushirikiana na raia...hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa na uchunguzi unaendelea,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Olomi alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii, wataanza utaratibu wa kuyalinda makanisa yote ili kuzuia matukio ya aina hiyo.

Mlinzi wa kanisa hilo Bw. Mussa Jackson, alisema awali alikimbilia vichakani ili kunusuru maisha yake na baadaye alikwenda kuomba hifadhi nyumba jirani iliyopo katibu na kanisa hilo.

“Wakati nikiwa lindoni, ghafla niliwaona watu watatu wanakuja ambao sikuwafahamu...nilipojaribu kuwafatilia wakaanza kurusha mawe hivyo nikaamua kukimbia,” alisema Bw. Jackson.

Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Penuel Wisdom alisema alipokea simu kutoka kwa Bw. Jackson ya kuchomwa kwa kanisa hilo ambapo thamani zilizoungua ni pamoja na viti, meza.

“Hii ni hujuma ya pili kufanywa katika kanisa letu ambapo mwaka 2011, kanisa hili lilivunjwa na watu wasiopungua 50, hasara iliyopatikana ilikuwa sh. milioni 20.

Wednesday, February 20, 2013

MAUAJI YA PADRI Z'BAR PENGO ATOA TAMKO ZITO

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
 










SIKU moja baada ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki la Minara miwili Zanzibar, kuuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika, Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo Kuu
la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ametoa tamko zito kwa Serikali.


Padri Mushi aliuawa juzi asubuhi wakati akishuka katika gari lake ili kwenda kuongoza ibaada katika Kanisa la Betras ambapo tayari Jeshi la Polisi nchini, limeanza uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo, wanakamatwa kwa gharama yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kardinali Pengo alivitupia lawama vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushindwa kuzuia mifarakano kati ya dini moja na nyingene.

Alisema vyombo hivyo vimeshindwa kusoma alma za nyakati kwani baada ya tukio la kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa kanisa hilo Parokia ya Mpendaye, Desemba 24,2012, wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar walisambaza vipeperushi vilivyokuwa na ujumbe uliokusudia kufanya jambo kubwa la uhalifu.

KAMPUNI YA GAME FRONTIERS YAFANIKIWA KUKAMATA PEMBE ZA NDOVU ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 192 WILAYANI NAMTUMBO MKOANI RUVUMA




Askari Wanyamapori wa pori la akiba Selou, wakiwa wameshika baadhi ya pembe za ndovu ambazo wamezikamata baada ya kuwakurupusha majangili waliokuwa nazo, wakitaka kutoroka nazo wilayani Namtumbo.





Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

KAMPUNI ya Game Frontiers Tanzania(GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na kikosi cha askari wanyamapori katika pori la akiba la Selou, wamefanikiwa kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya dola za kimarekani shilingi 120,000 sawa na fedha za kitanzania shilingi milioni 192.

Kaimu mkuu wa pori la akiba kanda ya kusini Magharibi Likuyuseka, Bernald Lijaji alisema tukio hilo lilitokea Februari 17 mwaka huu majira ya asubuhi, huko katika maeneo ya wazi jumuiya ya Mbarang'andu ambayo yamekaribiana na pori la akiba la Selou wilayani humo.
 

Lijaji alisema kwamba pembe zilizokamatwa zilikuwa 15 zenye  thamani ya fedha hizo, risasi tisa na bunduki mbili kati ya hizo moja ni aina ya Gobole na nyingine Raifo.

Tuesday, February 19, 2013

MAUAJI Z'BAR: PADRI MWINGINE APIGWA RISASI TATU KICHWANI, TIMU YA MAKACHERO YATUMWA, JK AOMBELEZA, WATATU MBARONI, WAUMINI WAANGUA KILIO

PADRI wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili, lililopo Mji Mkongwe, Zanzibar, Evaristus Mushi, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika jana asubuhi.
 
Tukio la mauaji hayo limeibua simanzi kubwa kwa waumini wa kanisa hilo ambao jana walikusanyika kanisani hapo baadhi yao wakilia, kulaani mauaji ya kinyama aliyofanyiwa kiongozi huyo.

Baadhi ya waumini hao, walihoji utekelezwaji wa tamko la Serikali baada ya Padri wa kanisa hilo, Parokia ya Mpendaye mjini Zanzibar, Ambrose Mkenda, kujeruhiwa kwa risasi Desemba 24,2012 na watu wasiofahamika akiwa nje ya nyumba yake.

Baada ya tukio hilo, Desemba 28,2012 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilitoa tamko la kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya mfululizo wa matukio ya kushambuliwa viongozi wa
dini ili kubaini kama ni hujuma zinazofanywa na baadhi  ya watu wanaotaka kuifanya Zanzibar isitawalike.

Monday, February 18, 2013

WAGENI WAKIONDOKA ENEO LA MJI MKONGWE JANA BAADA YA PADRI EVARIST MUSHI KUPIGWA RISASI NA KUFARIKI DUNIA

YALIYOJIRI ZANZIBAR:

Wageni wakikimbia eneo la mji mkongwe baada ya Padri Evarist Mushi, kupigwa risasi na kufariki dunia.(Picha na mtandao)

Saturday, February 16, 2013

MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA WAMLALAMIKIA WAKALA WA BARABARA MKOANI RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.











Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemjia juu wakala wa barabara za mkoa huo(TANROAD) kwamba, ameshindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za wilaya hiyo, ambazo ujenzi wake unasimamiwa na wakala huyo.

Licha ya baraza hilo kutoa malalamiko hayo kadhalika wameilalamikia TANROAD mkoani humo kwa kuwapa tenda za ujenzi wa barabara za wilaya ya Mbinga, makandarasi ambao hawana sifa na vifaa vya kutosha, ambavyo vingeweza kukidhi mahitaji halisi ya kujenga barabara kwa kiwango kinachotakiwa.

Malalamiko ya madiwani hao yalitolewa leo kwenye kikao cha kawaida cha baraza hilo, kilichoketi katika ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo Mbinga mjini.

Friday, February 15, 2013

BRUNO KAPINGA AWATAKA WANANCHI WAJENGE USHIRIKIANO


 Diwani wa Kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Bruno Kapinga (aliyevaa shati la kijani) akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtawa katika kata hiyo, ambapo alikuwa akiwataka washirikiane kwa pamoja katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa(maendeleo) husuani kupeleka watoto wao shule.(Picha na Kassian Nyandindi)

WAZEE WA KIJIJI CHA MTAWA WAKIPOKEA MSAADA WA CHAKULA KUTOKA KWA DIWANI WAO



Diwani wa kata ya Mkumbi Bruno Kapinga(aliyevaa kofia na shati la kijani) akiwa pamoja na wazee wa kijiji cha Mtawa kata ya Mkumbi wilayani Mbinga akisimamia zoezi la kugawa mihogo iliyomenywa vizuri, tayari kwa kusagwa kwa ajili ya kupata unga wa kupika ugali.(Picha na Kassian Nyandindi)

DIWANI KAPINGA ATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WALEMAVU, WAZEE NA WATU WASIOJIWEZA KATIKA KATA YA MKUMBI WILAYANI MBINGA

 Diwani wa kata ya Mkumbi Bruno Kapinga(aliyevaa shati la kijani) akikabidhi msaada wa gunia la mihogo iliyomenywa na kukaushwa vizuri tayari kwa kusagwa na kupata unga wa kupika ugali, kwa mtoto mwenye ulemavu wa miguu na mgongo Elekta Kapinga, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lugari katika kata hiyo. Wanaoshuhudia ni baadhi ya wazee ambao nao walipatiwa msaada huo wa chakula. (Picha na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SERIKALI imetakiwa kuendelea kuelimisha jamii iwajali na kuwaheshimu watu wenye ulemavu, wazee na watu wasiojiweza kama walivyo watu wengine katika kupata haki sawa, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo na kuondokana na migogoro isiyo ya lazima miongoni mwa jamii.

Rai hiyo ilitolewa na Diwani wa kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Bruno  Kapinga, alipokuwa akitoa msaada wa chakula kwa watu wenye ulemavu, wazee na watu wasiojiweza katika kata hiyo.

“Ndugu zangu hawa ni wenzetu ni lazima tuwajali katika hata kuwapatia misaada mbalimbali, tukiwatenga tutakuwa tunakosea hivyo tushirikiane pamoja”, alisema Kapinga.

Wednesday, February 13, 2013

WAKULIMA WA KAHAWA WASHAURIWA KUZINGATIA KANUNI ZA KILIMO BORA







Meneja wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kanda ya Ruvuma, Edmond Zani. (Picha na Kassian Nyandindi).











Na Kassian Nyandindi,
  
MOJA kati ya zao kuu la biashara linalozalishwa hapa nchini na kuuzwa nje ya nchi ni kahawa, ambapo zao hili huwasilisha kiasi cha asilimia tano ya bidhaa zinazouzwa nje na kuchangia kiasi cha asilimia 24 ya mapato ya nchi yanayotokana na kilimo.

Kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita zao la kahawa limekuwa linaingiza kiasi cha zaidi ya dola milioni miamoja za kimarekani na kwamba ni chanzo cha kipato kwa familia zipatazo 450,000 na limekuwa likinufaisha maisha ya watanzania wapatao milioni 2.5.

Katika nchi yetu ya Tanzania asilimia 90 ya zao hili huzalishwa na wakulima wadogo, ambapo kwa ujumla wastani wa uzalishaji kwa mwaka tani za kahawa safi ni 50,000 ukiambatana na kupanda na kushuka kila baada ya mwaka mmoja kati ya tani 68,000 na 33,000.

MGOGORO WA ARDHI WAIBUKA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MGOGORO umeibuka katika kata ya Utiri wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, baada ya wakazi wa kata hiyo kuilalamikia idara ya ardhi wilayani humo, kwa kutofuata taratibu za upimaji ardhi bila kushirikisha wananchi.


Malalamiko hayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara ulioketi mpakani mwa kata ya Utiri na Mbinga mjini, ambapo wakazi hao waliishutumu idara hiyo kwa kuingia eneo la kijiji cha Mtama katika kata hiyo na kuanza kupima ardhi, kwa lengo la kupanua eneo la mamlaka ya mji wa Mbinga.


Andrew Matteso mkazi wa kijiji cha Maumba alisema kitendo hicho ni sawa na ukiukwaji wa sheria zilizowekwa na serikali, hivyo wao wanachotambua eneo la mamlaka la mji huo, mpaka wake upo kati kati ya kitongoji cha kilosa na Maumba na kwamba wataalamu wa ardhi hawapaswi kupima ardhi hiyo kwa lengo la kupanua mji huo nje ya mpaka huo.

Saturday, February 9, 2013

MWENYEKITI JELA KWA KUTISHIA KUMUUA DIWANI


Na Steven Augstino,
Tunduru.

MWENTEKITI wa kata ya Nakapanya kwa tiketi ya Chama cha wananchi(UF)  Hassan Daimu Sinda, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 16 jela baada ya kupatikana ha hatia ya uchochezi na kosa la kutishia.


Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama  ya mwanzo Mlingoti mjini Tunduru baada ya kumtia hatiani katika makosa hayo ya kutishia kumuua  Diwani wa kata hiyo Mfaume Wadali, pamoja na kutoa tamko la kuwazuia wananchi kufanya kazi ya kujitolea yaliyofanyika Oktoba 28/2011.


Akitoa hukumu hiyo mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kuisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 21/2011 iliyohusu makosa ya kutishia kwa maneno kinyume na kifungu cha sheria namba 89 (2) (C) sura ya 16 kanuni ya adhabu na jinai namba 20/2011 ya kuwazuia wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo   kinyume cha kifungu
cha sheria namba 89 (2) (C)  sura ya 16 ya kanuni ya adhabu.

WANANCHI WA TUNDURU HAWANA BARAZA LA NYUMBA NA ARDHI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI Wilayani Tunduru Ruvuma imeahidi kufuatilia, kusimamia na kuhakikisha kuwa Baraza la ardhi na nyumba linaanzishwa wilayani humo ili kuwapunguzia kero wananchi wake.

Kauli hiyo imetolewa na katika sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria Tanzania, na mkuu wa wilaya ya Chande Nalicho wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya Wwilaya hiyo mjini Tunduru.

Kufuatia hali hiyo Nalicho akatumia nafasi hiyo kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kuangalia uwezekano wa kuingiza suala la uanzishaji wa baraza hilo katika bajeti zake, ili angalau kuanzisha ujenzi wa majengo yatakayotumika katika shughuli hizo za kutafsiri sheria na kutoa haki kwa walengwa.

WANA CCM WATAKIWA KUACHA UBAGUZI NA KUJENGA MAKUNDI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

VIONGOZI na Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Kata Mpya ya Majengo wilayani Tunduru Ruvuma, wamempongeza diwani wa kata hiyo Athumani Nkinde, kwa kuwafungulia miradi zaidi ya shilingi milioni 1.2 iikiwa ni juhudi za kuiendeleza kata yao.

Mwasisi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo Neema Chiwinga na Mwenyekiti wa kamati wa kikundi hicho Alus Chibwana ni miongoni mwa viongozi waliotoa pongezi hizo, wakati wakitoa ushuhuda wa maendeleo ya kata yao katika mkutano wa maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 36 toka kizaliwe yaliyofanyika kiwilaya katika kata hiyo.

Katika taarifa hiyo viongozi hao walimwelezea diwani Nkinde kuwa ni miongoni mwa madiwani wanaotakiwa kuigwa mfano, wilayani humo kutokana na upendo wake kwa wanachama na wakazi wote wa kata hiyo.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUTOA MIMBA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MHUDUMU wa kuuza vinjwaji katika baa ya Tunduru Pub mjini hapa, aliyefahamika kwa majina ya  Mary Baby Obodo amefariki dunia wakati akijaribu kutoa mimba kwa njia za kienyeji.

Binti huyo ambaye alianza kufanya kazi hiyo mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka jana katika baa hiyo, inadaiwa kuwa alifanya jaribio hilo la kutoa mimba wakati akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya iitwayo New Sety View ambako alikuwa akiishi tangu afike mjini hapa.

Wakizungumzia tukio hilo miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa baada ya kufanya jaribio hilo,  na kufanikiwa kuua kiumbe hicho marehemu alianza kuishiwa nguvu na kuzidiwa ghafla hali ambayo iliwafanya wasamaria wema kumkimbiza hospitali ya serikali ya wilaya ya Tunduru kwa matibabu zaidi.

DC TUNDURU AAHIDI KUFUNDISHA HESABU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Chande Nalicho ameahidi kuingia darasani na kuanza kufundisha somo la Hisabati katika shule ya sekondari ya kutwa ya Frenki Weston,  ikiwa ni juhudi za kuhakikisha  taalunma inaongezeka kwa wanafunzi katika shule hiyo.

Sambamba na taarifa hiyo ambayo alisema kuwa ni kupunguza ikama ya upungufu wa wafanyakazi wa idara ya elimu, pia ameahidi kuanzisha utaratibu wa kufanya ziara za kushitukiza katika shule zote wilayani humo ili kujionea hali halisi ya utendaji kazi ya walimu, ambao wanadaiwa kulegalega na kusababisha wilaya yake kufanya vibaya katika matokeo ya wanafuzi waliofanya mtihani wa kumaliza daraza la saba mwaka 2012.

Nalicho aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kutathimini hali ya maendeleo ya elimu wilayani Tunduru, Wilaya uliofanyika kwenye ukumbi wa kituo cha walimu (Klasta) mjini hapa huku akiongeza kuwa maamuzi ya kushika chaki na kuanza kufundisha yametokana na msukumo wa kusikitishwa na matokeo mabaya ya mtihani wa darasa la saba ingawa wanafunzi walitumia mfumo mpya wa kujibu maswa kwa kuchagua majibu.

MADIWANI TUNDURU WAPITISHA BAJETI YAO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la madiwani wa hlamashauri ya wilaya ya Tunduru Ruvuma limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya matarajio ya kukusanya na kutumia kiasio cha shilingi bilioni 34,425,566,350 katika kipindi cha mwaka  2013hadi 2014.

Akiwasilisha hivi karibuni taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Robert Nehatta katika kikao hicho kilicho fanyika ukumbi wa Klasta mjini hapa, afisa mipango wa wilaya hiyo Keneth Haule alisema kuwa kiasi hicho ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 6,881,058,813 sawa na asilimia 19.9% ikilinganishwa na bajeti ya shilingi. bilioni 27,544,507,537 zilizo idhinishwa katika bajeti ya mwaka 2012 hadi 2013.

Akifafanua taarifa hiyo Bw. Haule alisema kuwa katika ya fedha hizo Shilingi 34,425,566,350 zitatokana na makosanyo ya ndani vya halmashauri hiyo,Ruzuku ya matumizi ya kawaida tsh.18,174,302,120 Mishahara shilingi 18,868,732,200 na matumizi mengineyo (PE) ni Tsh.2,237,201,000.

BODI YA KOROSHO NA MWAROBAINI WA WALANGUZI WA ZAO HILO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BODI ya Korosho Tanzania imeahidi kutaifisha korosho zote ambazo hazitanunuliwa kupitia mfumo uliohalalishwa na serikali wa stakabadhi ghalani ikiwa ni juhudi ya kuendelea kulinda maslahi ya wakulima wa zao hilo.


Hayo yamebainishwa na bodi hiyo kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba CBT/M/1/VOL  XXV/40 ya Januari 23 mwaka huu, ambayo imesambazwa katika wilaya zinazolima korosho na kuongeza kuwa tamko hilo limetolewa kufuatia kuwepo kwa mfumuko wa walanguzi wazao hilo ambapo wakulima huwanyonya kupitia vipimo haramu vya Kangomba.


Barua hiyo iliyosainiwa na Teofora Nyoni  kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, ilibainisha kuwa  ili kufanikisha zoezi hilo pia amewaomba wakuu wa wilaya, wakurugenzi, viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kushirikiana na Jeshi la polisi kuwadhibiti na kuwakamata walanguzi hao.

ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUJERUHIWA NA MAMBA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI wa kijiji cha Muhuwesi wilayani Tunduru Ruvuma  Mustafa Kalesi(52) amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani humo baada ya kunusurika kifo na kujeruhiwa vibaya na Mamba.

Majeruhi Kalesi ambaye amelazwa katika kitanda namba 7 katika wodi namba moja akiwa hajitambui, alikumbwa hivi karibuni na mkasa huo wakati akijaribu kuoga katika mto Muhuwesi, ili aweze kurejea nyumbani kwake akitokea kutoka shambani.

Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na mashuhuda wa tukio hilo, walisema wakati akiendelea kuoga katika mto huo, ghafla alivamiwa na mamba huyo ambaye alianza kumshambulia  na kufanikiwa kumjeruhi vibaya.

Tuesday, February 5, 2013

BARAZA LA MADIWANI MBINGA NA NYASA LAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YAKE YA MAENDELEO YA WANANCHI KWA MWAKA 2013 / 2014

















Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oddo Mwisho(Kushoto) aliyevaa joho, wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani bcha mapendekezo ya mpango na bajeti kwa halmashauri ya wilaya ya Nyasa na Mbinga. Kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi akifuatilia kwa makini kitabu cha bajeti hiyo.( Picha na Julius Konala)



Na Julius Konala,
Mbinga.


BARAZA la Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, limepitisha jumla ya shilingi bilioni 65.9 kwa ajili ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hizo katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014.



Mapendekezo hayo yalipitishwa katika kikao cha baraza hilo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, na kuwasilishwa na kaimu ofisa mipango wa wilaya ya Mbinga Oscar Yapesa kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, chini ya Mwenyekiti wake Oddo Mwisho.



Yapesa alifafanua kwa kuanza na mapendekezo ya bajeti ya wilaya ya Nyasa, ambapo alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 28,842,596,431 zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya wananchi.



Kadhalika alieleza kuwa shilingi bilioni 37,073,888,863 nazo zitatumika kwa maendeleo ya wilaya ya Mbinga.

Saturday, February 2, 2013

MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA WAZUA MALALAMIKO

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WAKATI serikali ikiendelea kumaliza mgogoro wa kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, hali hiyo imehamia hapa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo juzi kundi la wakazi wa kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani humo, nalo lilikuja juu na kutaka kuandamana kwa muda wa masaa kadhaa kupinga kusafirishwa kwa makaa ya  mawe ambayo yanachimbwa kijijini humo.

Lengo la kutaka kufanya hivyo lilitokana na wakazi hao kudai nyongeza ya fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa maji katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini hayo.

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia kutokana na wachimbaji wa makaa hayo kutiririsha maji yenye mkaa wa mawe kuelekea kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe kama vile samaki kupoteza maisha ambapo serikali ya wilaya ya Mbinga baada ya kupata taarifa hizo, ilichukua jukumu la kwenda huko na kuamuru wachimbaji hao kuzuia maji hayo yasielekezwe katika mto huo.