Sunday, December 24, 2017

ASIMAMISHWA KAZI AKIDAIWA KUTENGENEZA MBINU CHAFU ZA KUTAFUNA MAMILIONI YA KAYA MASKINI



Na Muhidin Amri,         
Tunduru.

KAIMU Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chiza Malando amemsimamisha kazi Mtendaji wa kijiji cha Chilundundu wilayani humo, Timamu Issa kwa tuhuma ya kutengeneza mbinu chafu ya kutafuna mamilioni ya fedha za Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) katika kijiji hicho.

Sambamba na kumsimamisha kazi mtendaji huyo, Mkurungezi huyo amevunja kamati ya watu 14 ambayo ilikuwa ikisimamia utekelezaji wa mpango huo.

Malando alilazimika kuchukua hatua hiyo wakati alipokuwa akizungumza juzi na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika ukumbi wa Chama cha ushirika, Chiliwena Amcos ikiwa ni siku chache tu baada ya mbinu za viongozi hao kutaka kutafuna fedha hizo kubainika na wataalamu wa wilaya hiyo.


Alisema kuwa maamuzi hayo ameyachukua baada ya viongozi hao kubainika pia kutaka kuwaibia wanufaika wapatao 132 katika kijiji hicho zaidi ya shilingi milioni 1.8 ambazo zilipangwa kulipwa kwa wanufaika wa mpango huo.

Kufutia uwepo wa hali hiyo, Malando aliwataka walengwa wa mpango kufanya uchaguzi upya kwa kuteua wajumbe wapya ambao wataweza kuongoza kwa kufuata taratibu husika.

Alisema kuwa kulingana na maelekezo ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano, haiwezekani kuendelea kuwavumilia viongozi wa mtindo huo ambao wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya wananchi wenzao na kuigombanisha Serikali na wananchi wake.

“Mtendaji huyu asimame kazi kuanzi leo hii ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili”, alisema.

Malando aliongeza kuwa tume atakayounda kuchunguza jambo hilo itafanya kazi kwa haraka na ikibainika kuwa ni kweli hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Awali akitoa taarifa hiyo Mratibu wa TASAF wilaya ya Tunduru Emmanuel Luhanzu alisema kuwa njama za kutaka kuiba fedha hizo ziligundulika wakati wa malipo yaliyofanyika Desemba 5 mwaka huu, baada ya wasimamizi wa malipo ya mradi huo kutoka katika kijiji hicho (CMC) kuonekana wakitumia muda mwingi kufanya hesabu za malipo ya mnufaika mmoja.

Alisema baada ya kulibaini hilo alisogea taratibu hadi katika meza ya kulipia na kubaini uwepo wa karatasi nyingine nje ya karatasi ambayo ilipelekwa na TASAF wakati wa kuandaa malipo hayo.

Alisema katika kuhakikisha kuwa wanafanikisha mbinu za wizi huo zinafanikiwa mtendaji huyo alifika katika kituo cha malipo hayo akiwa amelewa na kuanzisha vurugu jambo ambalo lilileta taharuki kwa wanufaika hao.

Naye Mratibu wa mpango huo wilayani hapa, Muhidin Shaibu aliwahimiza walengwa hao kufanyia kazi haraka maelelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi mtendaji, Malando kwa kuchagua haraka kamati mpya ambayo itasimamia kikamilifu ili kuwezesha mpango huo kuweza kuendelea vizuri.

Shaibu alisema kuwa endapo watashindwa kutekeleza maelekezo hayo upo uwezekano wa kuufuta mradi huo katika kijiji chao na kupelekwa katika vijiji vingine na kwamba Mfuko huo wa maendeleo ya jamii unatekeleza mradi huo katika vijiji 88 tu wilayani Tunduru na kwamba vijiji vingine 66 havijapelekewa mradi huo.

No comments: