Sunday, December 31, 2017

WAKAZI 100 KIGONSERA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUKATAA KUSHIRIKI SHUGHULI ZA MAENDELEO


Na Muhidin Amri,       
Mbinga.
 
JUMLA ya Wakazi 100 wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamefikishwa Mahakamani kwa kosa la kukataa kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi.

Hayo yalisemwa juzi na Mtendaji wa kata ya Kigonsera, Raphael Kalembo wakati alipokuwa akizungumzia ujenzi wa nyumba moja ya walimu katika shule ya Sekondari ya Kigonsera ambayo ujenzi wake ukikamilika, itakuwa na uwezo wa kuishi walimu watakaoweza kufanya kazi ya kufundisha katika shule hiyo.

Ujenzi wa nyumba hiyo ni mkakati wa uongozi wa shule kwa kushirikiana na halmashauri hiyo kutatua kero ya nyumba za kuishi walimu hao katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga.


Kalembo alisema kuwa kati ya hao tayari wengine wamekwisha hukumiwa vifungo na baadhi wamelipa faini kama hatua ya kuwataka kutambua majukumu na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kazi za ujenzi wa taifa.

Alisema kuwa kazi ya ujenzi wa Taifa ni jukumu la kila mmoja katika jamii lakini moja kati ya changamoto zinazoikabili kata hiyo ni baadhi ya wananchi kukataa kushiriki shughuli za maendeleo, hivyo kusababisha kata hiyo kuwa na miradi mingi viporo ikilinganishwa na kata nyingine.

Tatizo la upungufu wa nyumba za kuishi walimu katika shule hiyo na shule nyingine zilizopo kwenye kata hiyo limekuwa kubwa hivyo zinahitajika juhudi kubwa kuhakikisha kwamba wanajenga haraka nyumba za kutosha ili kuweza kuwaondolea kero ya walimu kupanga uraiani.

Alifafanua kuwa mbali na ujenzi wa nyumba hizo halmashauri hiyo ya wilaya inaendelea na ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi katika shule ya Sekondari Kiamili iliyopo katika kata hiyo, ambayo kila moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 48 ili kuwasaidia wasiweze kuishi mbali na mazingira ya shule.

Kwa upande wake Kaimu Afisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Zainabu Mfinanga alitolea ufafanuzi kuwa kazi ya ujenzi wa mabweni hayo unaenda sambamba na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule na nyumba hizo za walimu katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

No comments: