Sunday, December 24, 2017

WANAOTOA HUDUMA YA KUUZA CHAKULA TUNDURU KUPIMWA AFYA ZAO


Na Muhidin Amri,        
Tunduru.

MGANGA Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Dokta Wendy Robert amesema kuwa idara ya afya katika wilaya hiyo itaanza kupima afya za wananchi wanaotoa huduma ya kuuza chakula katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Akizungumza juzi na baadhi ya watoa huduma alisema kuwa lengo la mpango huo ni kuhakikisha  kuwa kila mtoa huduma anakuwa na afya njema, ili kuepusha uwezekano wa kuambukiza wateja wao hasa pale wanapowahudumia ili kupata watu wenye afya njema watakaoweza kushiriki moja kwa moja katika kazi za maendeleo.

Aidha alisema kuwa zoezi hilo litafanyika kwa wilaya yote ya Tunduru katika migahawa, hoteli na maeneo mengine kwani wapo baadhi ya watoa huduma kama vile kwenye migahawa bado hawajapimwa afya zao jambo linaloweza kuhatarisaha maisha ya watu wengine.


“Unapokuwa na matatizo ya kiafya kama vile TB na magonjwa mengine ni rahisi kuambukiza watu wengine kwa njia ya hewa, kwa hiyo tunataka kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wa chakula wanakuwa na afya njema”, alisema Dokta Robert.

Katika utekelezaji wa mpango huo, alisema timu ya wataalamu wa afya itatembelea katika kila kata ili kuweza kuleta ufanisi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo na kwamba wamiliki wa migahawa na hoteli wametakiwa pia kuwafanyia uchunguzi wa afya wafanyakazi wao mara kwa mara.

No comments: