Wednesday, December 27, 2017

MAHANJE MADABA KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda akikagua chanzo cha maji ambacho kitatumika kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji unaojengwa na Serika ili kuweza kuwanufaisha wakazi wa kijiji cha Mahanje wilayani humo waweze kuondokana na kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda upande wa kulia, katikati Kaimu Mhandisi wa maji wa wilaya hiyo Makarius Nyoni wakiangalia mabomba yanayoendelea kusambazwa kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika kijiji cha Mahanje kata ya Mahanje ambao unalenga kumaliza kero ya maji kwa wakazi  wa kijiji hicho.


Na Muhidin Amri,       
Madaba.

WAKAZI 2,196 wanaoishi katika kijiji cha Mahanje kata ya Mahanje Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji ambao ujenzi wake unagharimiwa na Serikali, ambapo mara baada ya kukamilika kwake unalenga kumaliza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi hao.

Akizungumza katika eneo la mradi huo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Shafi Mpenda alisema Serikali imetoa shilingi milioni 275 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu na kwamba utakamilika mwishoni mwa mwezi Februari mwakani 2018.

Mpenda alisema kuwa hapo awali wananchi wa kijiji hicho walibuni mradi wao wa maji kwa ajili ya kumaliza kero ya maji, hata hivyo kutokana na ongezeko la kaya ilisababisha kuwepo kwa upungufu wa maji na Serikali ikaona ni vyema sasa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma hiyo ili wananchi wengi waweze kunufaika na hatimaye kuondokana na kutumia muda wao mwingi kufuata huduma hiyo umbali mrefu.


Kadhalika Mkurugenzi huyo alimshukuru Rais Dokta John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa fedha hizo za kutekeleza mradi huo ambao utamaliza kero ya muda mrefu ya maji kwa wakazi wa kijiji cha Mahanje na maeneo mengine jirani na kijiji hicho.

Mpenda amemuagiza mkandarasi anayejenga mradi huo Kampuni ya Kipera Construction Company Limited ya kutoka Songea, kuhakikisha kwamba inafanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha mradi kwa wakati na sio vinginevyo.

Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo, David Alli aliongeza kuwa kazi hiyo wanatarajia kuikamilisha baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa kwani tayari wamekwisha tega mabomba kutoka kwenye tenki kubwa hadi kwenye chanzo cha maji.

No comments: