Saturday, December 9, 2017

HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA KUENDELEA KUUNGA MKONO MAENDELEO YA WANANCHI WAKE

Aliyesimama ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kibanga wilayani humo ambao hawapo pichani wakati alipokuwa katika eneo la ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho. 
Jiwe la msingi ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kibanga kata ya Muji wilayani Mbinga likiwekwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gombo Samandito ambapo ujenzi huo umefanyika baada ya wananchi kujitolea nguvu zao kujenga jingo hilo la zahanati na kwamba Serikali imetoa vifaa vya kiwandani bati, saruji na nondo ili kuweza kukamilisha ujenzi huo.


Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito akiweka jiwe la msingi ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Myau kata ya Mbuji wilayani humo baada ya wananchi kujitolea nguvu zao ambapo ujenzi wa zahanati hiyo Mkurugenzi huyo aliweza kutoa vifaa vya kiwandani bati, saruji na nondo ili kuweza kukamilisha ujenzi huo. 



Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gombo Samandito amesema kuwa zoezi la kusambaza vifaa vyote vya kiwandani katika miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini, halmashauri hiyo itaendelea kuvisambaza ili kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa katika jamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Samandito alisema hayo juzi wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Kibanga na Myau zilizopo katika kata ya Mbuji kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye.

Alisema kuwa pale ambapo nguvu ya wananchi inaonekana katika ujenzi wa mradi wowote wenye manufaa kwa umma, Serikali nayo ni lazima ichangie nguvu yake ili mradi husika uweze kukamilika kwa wakati na hatimaye ulete manufaa katika jamii.



Kadhalika katika kata hiyo alisisitiza kuleta vifaa vya kiwandani ili kuweza kumalizia ujenzi wa bweni la kulala wanafunzi katika shule ya Sekondari Mbuji ambayo tayari wananchi wake wameweza kuonyesha nguvu zao za ujenzi wa jengo hilo.

“Ndugu zangu vifaa vya kiwandani kama vile nondo, simenti na vinginevyo pale vinapohitajika tuwasiliane ni lazima tuvilete katika kukamilisha ujenzi wa miradi hii ya wananchi, hivyo naagiza viongozi wenu waje kuvichukua ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyojiwekea katika kukamilisha miradi hii”, alisisitiza Samandito.

Awali kwa mujibu wa taarifa ya maendeleo ya wananchi hao juu ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Kibanga na Myau na bweni hilo la kulala wanafunzi katika shule hiyo, inaeleza kuwa wameweza kuungana pamoja kufyatua tofari, kuchangishana fedha na kuweza kujenga majengo hayo ambayo sasa yanahitaji nguvu ya Serikali kwa ajili ya kuweza kupata vifaa vya kiwandani ili yaweze kukamilika ujenzi wake.

Kwa upande wao wananchi hao walimshukuru Samandito kwa jitihada anazozifanya za kuunga mkono nguvu hizo za wananchi katika kusambaza vifaa hivyo vya kiwandani katika kuweza kukamilisha miradi ya maendeleo ya wananchi. 



 

No comments: