Saturday, December 23, 2017

TUNDURU NA MKAKATI WA KUPUNGUZA VIFO VYA AKINA MAMA WAJAWAZITO



Na Muhidin Amri,    
Tunduru.

JUMLA ya akina mama 16 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja, kutoka Januari mwaka jana hadi kufikia Desemba mwaka huu kutokana na matatizo mbalimbali wakati walipokuwa wakijifungua wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Imefafanuliwa kuwa vifo hivyo vimesababishwa na mimba kutunga nje ya mirija ya uzazi, kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua na upungufu mkubwa wa damu kwa akina mama wanaokwenda kujifungua hospitali.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mratibu wa huduma ya  afya, uzazi na mtoto wilayani humo, Salome Namlia alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu Ofisini kwake.


Namlia alibainisha kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu wajawazito 10,714 sawa na asilimia 81 walihudhuria kliniki na kwamba waliojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma walikuwa 8,852 sawa na aslimiia 67.

Alisema kuwa wastani wa vifo vya akina mama wajawazito wilayani hapa ni 124 kati ya 100,000 lakini bado juhudi zinafanyika kuhakikisha kwamba idadi hiyo inapungua hadi kufikia 100 kwa 100,000.

Kadhalika katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru jumla ya vituo vinavyotoa huduma ya afya ya  uzazi ni 61 na kwamba huduma ya kujifungulia vipo 60 ambapo hospitali ni tatu, vituo vya afya vitano na zahanati 53.

Vilevile kutoka mwaka 2016 hadi  Novemba 2017 jumla ya watoto 10,354 walizaliwa ambapo kati ya hao watoto waliozaliwa hai walikuwa 9,087 waliozaliwa pacha walikuwa 234 na watoto waliozaliwa uzito pungufu walikuwa 1,033 ambao ni sawa na  asilimia 12.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dokta Wendy Robert alisema huduma za uzazi wa mpango zinazotolewa katika vituo vyote 65 vya kutolea huduma za afya katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru katika kipindi cha 2016/2017 jumla ya wateja 21,166 waliandikishwa na kuanza kutumia njia mbalimbali za uzazi wa mpango.

Pia alieleza kuwa upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) ulifanyika katika vituo 62 vya kutolea huduma za afya kwa kila mama mjamzito na kila anayehudhuria Kliniki na kwamba katika kipindi hicho akina mama wajawazito 10,714 walipimwa. 

Dokta Robert alisema kuwa kuanzia mwezi Julai hadi Septemba  mwaka huu pia akina mama 3,027 walipimwa na 91 walikutwa na VVU hata hivyo changamoto kubwa iliyopo sasa ni uhaba wa watumishi wenye taaluma hasa katika vituo vya afya na zahanati pamoja na mwitikio mdogo wa wenza wao kwenda Kliniki kupima afya zao.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, halmashauri imeendelea kutenga fedha katika bajeti yake ya kila mwaka kwa ajili ya kuajiri watumishi wenye taaluma ya afya na kufanya uhamasishaji wa kutoa elimu kwa kuwahimiza akina mama wajawazito kuwahi kliniki mapema kupima afya zao.

No comments: