Tuesday, December 19, 2017

VYETI FEKI TUNDURU UHABA MKUBWA WATUMISHI IDARA YA AFYA



Na Mwandishi wetu,   
Tunduru.

ZOEZI la kutambua watumishi  wenye vyeti feki lililofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dokta John Magufuli, limesababisha idara ya afya katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuwa na upungufu wa watumishi 947 sawa na asilimia 73.7 wa kada mbalimbali ambao wanahitajika kufanya kazi katika  vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo.

Hayo yalisemwa na mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dokta Wendy Robert alipokuwa akizungumza juzi na mwandishi wetu Ofisini kwake ambapo alisema kada inayoongoza kuwa na upungufu mkubwa ni maafisa tabibu (CO) kwani  mahitaji halisi ni 110 na waliopo ni 10 tu.

Aidha Dokta Robert alieleza kuwa eneo lingine lenye upungufu ni maafisa tabibu wasaidizi (ACO) madaktari, madaktari wasaidizi na kwamba huwalazimu waliopo kwa uchache wao  kufanya kazi bila kupumzika ili kuwatendea haki wananchi wanaofika  kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.


Dokta Robert aliyataja maeneo mengine yanayokabiliwa na upungufu huo  kuwa ni idara ya meno, famasia, Daktari wa meno msaidizi (ADO) maafisa wauguzi, wateknolojia wasaidizi, kitengo cha maabara, mionzi na maafisa afya.

Vilevile katika mwaka 2017/2018 alisema idara ya afya imepokea watumishi wapya saba kati ya tisa waliopangiwa kufanya kazi katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru, hata hivyo kati ya hao watumishi saba walioripoti mtumishi mmoja anayo hitilafu ya uwiano wa vyeti na kada aliyopangiwa.

Dokta Robert alisema licha ya upungufu huo wa wataalamu na watumishi wa sekta ya afya Serikali inaendelea na ujenzi wa wodi mbili katika hospitali hiyo ya wilaya na zahanati moja katika kijiji cha Legezamwendo.

Katika kuunga mkono jitihada hizo zinazofanywa na Serikali wananchi nao wameanza  ujenzi wa kituo cha afya Nakayaya kwa nguvu zao ili kuweza kuwarahisishia upatikanji wa huduma za afya jirani na maeneo yao wanayoishi.

Katika hatua nyingine Dokta Robert alisema idara ya afya katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru ina jumla ya vituo 65 vya kutolea huduma za afya zikiwemo hospitali tatu kati ya hizo moja ni ya Serikali na mbili za mashirika ya dini, vituo vya afya vitano ambavyo vyote vinamilikiwa na Serikali na zahanati mbili ambazo zinamilikiwa na watu binafsi.

Alisema kutokana na mpango wa Maendeleo  ya Afya ya Msingi (MMAM) unaoelekeza uwepo wa zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya kwa ngazi ya kata, halmashauri hiyo inaendelea kuimarisha zahanati zake kwa kuwa tayari kila kijiji kina zahanati.

No comments: