Wednesday, December 27, 2017

JAMII YATAKIWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU UJENZI WA MABWENI KIAMILI SEKONDARI MBINGA


Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

BAADHI ya Wanafunzi wanaosoma shule ya Sekondari Kiamili iliyopo katika kata ya Kigonsera Halmashauri Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, wameiomba jamii kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali yao ya awamu ya tano katika kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo hasa katika ujenzi miundombinu mbalimbali kama vile mabweni ya kulala wanafunzi.

Shule hiyo ambayo ina watoto zaidi ya 800 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa vyumba vya kulala wanafunzi jambo ambalo limesababisha baadhi ya wanafunzi wa kike sita kwa nyakati tofauti kupata ujauzito na kukatisha masomo yao.

Wakizungumza na mwandishi wetu, baadhi ya wanafunzi waliokutwa shuleni hapo wakiendelea na masomo yao wakati huu wa likizo walisema kuwa, uhaba wa mabweni ni changamoto kubwa kwao hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao wanaishi mbali na eneo la shule na hujikuta wakiingia katika vishawishi vya ngono.


Esta Kinyero ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu alisema kuwa tatizo hilo la kuishi umbali mrefu na mazingira ya shule, limekuwa likichangia pia baadhi yao kukosa hata muda wa kuhudhuria vipindi vya masomo shuleni kwa wakati.

Naye Saveria Kitusi aliongeza kuwa changamoto hiyo ya ukosefu wa mabweni imekuwa ikichangia hata wanafunzi wengine kujiingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu na kutozingatia ipasavyo taaluma shuleni.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Kiamili, Frank Kinunda alibainisha kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo halmashauri ya wilaya ya Mbinga imeanza kujenga mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wa kiume na wasichana.

Kinunda alisema pamoja na ujenzi huo wa mabweni unafanyika lakini bado hayatoshelezi mahitaji kwani yatakuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 46 tu badala ya watoto 98 kwa kila bweni kama ilivyokusudiwa.

Alieleza kuwa tayari wamepokea mifuko 100 ya saruji, nondo bati na misumari kutoka halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo lakini bado kumekuwa na tatizo la jamii kutoshiriki kikamilifu kwa kujitolea nguvu zao katika shughuli hizo za ujenzi.

No comments: