Friday, December 29, 2017

UJENZI MABWENI MAHANJE MADABA KUSAIDIA KUMALIZA KERO WANAFUNZI WANAOSOMA MBALI NA SHULE


Mkuu wa shule ya Sekondari Mahanje Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Marcelino Kilewa upande wa kulia akimounesha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda madawati yaliyotengenezwa ambayo ni kwa ajili ya maandalizi ya  kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza wanaotarajia kujiunga na shule hiyo mara shule zitakapofunguliwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda upande wa kushoto akiangalia ukuta wa jengo moja kati ya mabweni mawili yanayojengwa katika shule ya Sekondari Mahanje  kata ya Mahanje ambapo kulia kwake ni Mkuu wa shule hiyo, Marcelino Kilewa.

Na Muhidin Amri,      
Madaba.

UJENZI wa mabweni ya kulala Wanafunzi katika shule ya Sekondari Mahanje, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma utasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza kero ya watoto wanaosoma katika shule hiyo kutembea umbali mrefu wa kilometa 12 kutoka majumbani kwao hadi shuleni.

Hivi sasa ujenzi huo ambao unaendelea kufanyika ni wa mabweni mawili makubwa yanajengwa ambayo kila moja litakuwa na uwezo wa kulaza watoto 80.

Shule hiyo ambayo ni ya wasichana na wavulana, yanajengwa majengo hayo kwa ajili ya kulaza watoto hao ambayo sasa yamefikia hatua ya mwisho kukamilika kwake na kwamba, yataweza pia kusaidia hata wanafunzi hao wasiweze kupoteza muda wao wa kuhudhuria ipasavyo vipindi vya masomo darasani.


Mbali na kumaliza kero hiyo mabweni hayo yatasaidia kuongeza ukuaji wa taaluma kutokana na watoto wengi wataishi katika mazingira ya shule na kupata muda mwingi wa kujisomea tofauti na ilivyokuwa sasa.

Mkuu wa shule hiyo, Marcelino Kilewa alisema Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 196.8 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo, vyumba viwili vya madarasa na matundu ya choo katika shule hiyo.

Alisema kuwa katika mwaka wa masomo 2018, shule hiyo inatarajia kupokea wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza 135 na tayari kuna wanafunzi 247 ambao wanasoma wakitokea majumbani kwao.

Kwa upande wake Afisa elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Davis Mwasi aliongeza kuwa mradi huu wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa na matundu ya vyoo unalenga zaidi kuinua maendeleo ya elimu kwa watoto hao.

Alisema kuwa Serikali imetoa fedha hizo ambapo miundombinu hiyo ujenzi wake umefikia hatua nzuri na halmashauri hiyo tayari imejipanga kwa kila shule ya Sekondari wilayani humo kunakuwa na mabweni ya kutosha kwa ajili ya kulala wanafunzi.

Hata hivyo Afisa elimu huyo amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Madaba, Shafi Mpenda kwa juhudi zake anazozifanya za ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali wilayani hapa.

No comments: