Sunday, December 10, 2017

MLIPUKO UGONJWA WA KIPINDUPINDU NYASA UMESABABISHWA NA KUTOZINGATIA KANUNI BORA ZA USAFI

Baadhi ya Wananchi wa wilaya ya Nyasa wakiwa pembezoni mwa ziwa Nyasa.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

TIMU ya Wataalamu wa Wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto imebaini kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ambao umetokea katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, umesababishwa na wakazi wanaoishi katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo kutozingatia kikamilifu kanuni bora za usafi katika mazingira yao wanayoishi.

Kufuatia hali hiyo, vifo vya watu nane vilijitokeza kutokana na ugonjwa huo kati ya wagonjwa 185 waliojitokeza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Liuli, Kituo cha afya Lundo, Chiulu na Mbamba bay.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa huo, Dokta Gosbert Mutahyabarwa alisema kuwa upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu hao umebaini kuwa kati ya sampuli 15 zilizochukuliwa katika maeneo ambayo ugonjwa huo umetokea, sampuli 13 zilikuwa na vimelea vya Kipindupindu.

Dokta Mutahyabarwa alifafanua kuwa kata ambazo zilikuwa zimeathiriwa na ugonjwa huo ni Mtipwili, Chimate na Lipingo wilayani humo.

Alieleza kuwa chanzo cha mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu kilitokana na familia ya Filbert Nchimbi kuanza kutapika na kuharisha kinyesi cha njano ambapo walipelekwa kituo cha afya Mbamba bay na kubaini dalili za tatizo hilo.

Pia alisema kuwa mwanafunzi wa miaka tisa ambaye ni wa darasa la tatu naye alipelekwa katika kituo hicho cha afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini baadaye alifariki dunia.

Kadhalika alisema sababu kuu ya chanzo cha tatizo hilo katika maeneo hayo kimetokana na watu kunawa mikono katika chombo kimoja wakati wa kula, baadhi ya nyumba kutokuwa na vyoo na nyumba nyingine vyoo vilikuwa vimejaa, upungufu wa maji ya bomba, kula chakula bila kunawa mikono, uwepo wa migahawa ya kuuza chakula bila kufuata kanuni za usafi.

Dokta Mutahyabarwa aliongeza kuwa sababu nyingine ni wakulima wa kilimo cha mpunga kujisaidia ovyo katika mashamba yao na kusababisha mvua zinazonyesha masika hii kutiririsha uchafu kwenye makazi ya watu na vyanzo vya maji, unywaji wa pombe za kienyeji bila kuzingatia kanuni za usafi wakiwa katika mazingira machafu na wavuvi kuwa na mazoea ya kujisaidia katika vyanzo vya maji.

Hata hivyo mwito umetolewa kwa wananchi wa wilaya ya Nyasa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo wanapaswa kuzingatia kanuni bora za usafi ili kuweza kunusuru afya za wengine zisiweze kuathiriwa na Kipindupindu.

No comments: