Sunday, December 17, 2017

WANANCHI MINDU TUNDURU WAONDOKANA NA ADHA YA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA


Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkaoni Ruvuma, Chiza Malando na Mwakilishi wa Serikali ya Canada, Harkiran Rajasans kwa pamoja wakikata utepe kufungua kisima cha maji katika kijiji cha Mindu kata ya Mindu wilayani Tunduru.
Na Kassian Nyandindi,      
Tunduru.

KIJIJI cha Mindu kilichopo katika kata ya Mindu Wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wakazi wake wanaoishi katika kijiji hicho wameondokana na shida ya upatikanaji wa maji safi na salama, baada ya uongozi wa Kanisa la Anglikana jimbo la Masasi kuwajengea kisima kikubwa cha maji.

Imeelezwa kuwa ujenzi wa kisima hicho, Kanisa lilitekeleza mradi huo kupitia mradi wa Uboreshaji wa afya ya mama na mtoto (CHIP).

Wakizungumza baada ya kuzinduliwa ujenzi wa kisima hicho, baadhi ya wanawake wa kijiji hicho mbali na kupongeza juhudi zilizofanywa na uongozi husika walisema hivi sasa hata ndoa zao nyumbani wanakoishi kijijini humo zitakuwa salama kwa kuwa hawataweza kutumia muda mrefu kutafuta huduma ya maji mbali na makazi yao.


Debora Mambo na Joyce Daud kwa nyakati tofauti walisema kuwa awali ilikuwa ikiwalazimu kutoka majumbani mwao majira ya saa nane usiku na kurudi  majira ya saa 11 alfajiri wakitoka kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali nyumbani jambo ambalo lilikuwa likisababisha migogoro mingi kwenye ndoa zao.

Walisema maisha ya wananchi wa kijiji hicho hasa wanawake yalikuwa magumu kutokana na ukosefu wa huduma hiyo kwa sababu wakati mwingine walikuwa wakikosa hata nafasi ya kufanya shughuli zao za maendeleo.

Kwa upande wake Mratibu wa CHIP, Geofrey Monyesa amewashukuru watumishi wa halmshauri ya wilaya ya Tunduru kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kufanya utafiti wa ujenzi wa mradi huo na hatimaye kufanikiwa kuchimba kisima ambacho sasa kitawaondolea kero ya maji iliyodumu kwa muda mrefu katika kijiji hicho.

Alisema mradi wa kisima cha maji katika kijiji cha Mindu ni kati ya miradi 24 ya visima vya maji vilivyotekelezwa katika wilaya ya Masasi ambayo imepata kisima kimoja na Tunduru visima 23 ambapo lengo lake ni kuwapunguzia wasichana waliopo shuleni na wanawake majumbani kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

Monyesa alifafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Kanisa la Anglikana jimbo la Masasi, itasaidia  wanafunzi wa kike kupata muda mwingi wa kuhudhuria masomo darasani na muda wa kujisomea pale wanaporudi nyumbani.

Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Malando aliongeza kuwa kufunguliwa kwa kisima cha maji ni kati ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na wafadhili wa ndani na nje ya nchi katika mkakati wake kuboresha maisha ya Watanzania.

Aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na wafadhili pamoja na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwatoa katika adui wa maradhi, umaskini na ujinga huku akisisitiza kuwa mpango wa Serikali ya awamu ya tano ni kuona kila mmoja anapata maji safi na salama.

Malando aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali yao iliyopo madarakani kwa kufanya kazi za kujitolea kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule, barabara, maji na afya badala ya kuendelea kuwa walalamikaji jambo ambalo linachelewesha kukua kwa maendeleo yao.

No comments: