Sunday, December 24, 2017

WAZIRI MKUU AWATOA HOFU WAKAZI WA SONGEA JUU YA KULIPWA FIDIA WANAYODAI BILIONI 3.8


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia jana wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika Manispaa ya Songea ambako alienda kusikiliza kero yao ya muda mrefu ya kutolipwa fidia katika ardhi yao ambayo imetwaliwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanadai fidia ya shilingi bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na kuwa eneo la kiuchumi mkoani humo (Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Amewatoa hofu jana wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Manispaa hiyo.

Majaliwa alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inatambua kilio chao ambacho alisema ni cha muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa Mbunge wao wa zamani, Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu ili kuweza kumaliza jambo hilo.


“Alipotoka kutibiwa India alikuja Ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi, la kwanza lililkuwa ni hili la fidia kwa wakazi wa Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi wa kituo cha mabasi cha mjini Songea,

“Leo nimefanya ziara maalum kwa ajili yenu kwa sababu Serikali ya awamu ya tano ipo kwa ajili yenu na hasa wananchi wanyonge na tatizo hili inalijua kabla sijafika hapa, nilipita kwenye eneo husika na afisa mipango miji akanionyesha ramani ya eneo lenu hili”, alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo aliwaeleza pia wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu. 

Alieleza kuwa kutakuwa na kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na mbolea na kwamba kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha kukamua mafuta ya mbegumbegu huku akiongeza kuwa  hata ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba bay wilayani Nyasa mkoani hapa inatarajiwa kupita kwenye eneo hilo.

Vilevile akitoa ufafanuzi juu ya kuchelewa kwa malipo yao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba kati ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.

Kadhalika alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa ulipaji huo kwa sababu walifuata orodha ya majina (Kialfabeti) badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika. 

“Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe, Serikali itawafuatilia hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia waweze kulipwa”, alisema.

Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni shilingi 3,254,737,622 ambapo kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 shilingi 1,920,242,121 ambapo kati ya hizo, shilingi 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za wananchi na shilingi 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika. 

Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,033 (Sawa na ekari 5,000) lilitwaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea tangu mwaka 2007 na kwamba eneo hilo linajumuisha mitaa ya Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na Luhira.

No comments: