Sunday, December 31, 2017

MJI WA MBINGA WAENDELEA KULALAMIKIA UCHAFU WAMSUBIRI KWA HAMU WAZIRI MKUU


Uchafu ukiwa umezagaa katika baadhi ya maeneo ya makazi ya watu mji wa Mbinga mkoani Ruvuma kama ulivyokutwa leo na mpiga picha wetu ambapo baadhi ya wakazi wa mji huo wameonesha kukerwa na uchafu huo na kuutaka uongozi wa Halmashauri ya mji wa Mbinga kutatua kero hiyo haraka ambayo imedumu kwa muda mrefu kabla hayajatokea madhara makubwa. (Picha zote na Muhidin Amri)


Na Muhidin Amri,     
Mbinga.

BAADHI ya Wananchi wa Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wameitaka Halmashauri ya mji huo kuongeza kasi katika suala la kufanya usafi wa mazingira ili kuweza kuepusha uwezekano wa kutokea magonjwa mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu hasa kipindi hiki cha masika.

Walisema kuwa kwa muda mrefu halmashauri hiyo imekuwa ikisuasua katika masuala ya utekelezaji wa usafi wa mazingira ya mji huo katika maeneo mbalimbali, huku watendaji wake wenye dhamana wakiona mlundikano wa uchafu mitaani na kushindwa kuchukua hatua madhubuti ya kumaliza tatizo hilo.

John Mapunda ambaye ni mkazi wa mtaa wa Kipika alisema kuwa kipindi hiki ni cha  masika na ndiyo muda ambao hatari zaidi kwa magonjwa ya mlipuko, hivyo Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Kadaso Mageni kwa kushirikiana na wataalamu wake wa masuala ya usafi wa mji huo wanapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea hapo baadaye.


Alisema mji wa Mbinga  ni mdogo lakini uzalishaji wa taka umekuwa mkubwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu hasa wafanyabiashara ndogondogo na mama lishe ambao wamekuwa wakitupa taka hovyo na usimamizi wa kudhibiti tatizo hilo mitaani umekuwa mdogo.

Ester Komba alisema hata uchafu unaotupwa kwenye maghuba bado ni tatizo kubwa kwa sababu umekuwa ukikaa kwa muda mrefu bila kuzolewa na kufikia hatua ya kuoza na kutoa harufu na kuwa kero kwa wananchi.

Komba alisema kuwa wanamsubiri kwa hamu kubwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili wamueleza kero hiyo na matatizo mengine yanayoendelea kuwa kero kwao na yanaonekana baadhi ya viongozi wa mji huo muda mwingi kujali maslahi yao binafsi badala ya kuwatumikia wananchi.

Alisema kuwa ni aibu kubwa mji wa Mbinga ambao una wananchi wenye nguvu kubwa ya kiuchumi kuwa mchafu jambo ambalo linaonesha kuwa hata Mkurugenzi wake anayeongoza mji huo kushindwa kusimamia kikamilifu baadhi ya majukumu aliyopewa na Serikali.

Hata hivyo jitihada za mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mkurugenzi mtendaji wa mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni ili aweze kutolea ufafanuzi wa kero hiyo hakuweza kupatikana Ofisini kwake na pale alipopigiwa simu ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: