Saturday, December 30, 2017

MADABA WATAKIWA KUSHIRIKI VYEMA KATIKA SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO

Na Mwandishi wetu,    
Madaba.

MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amewataka wananchi wa Jimbo la Madaba kuhakikisha kwamba wanashiriki vyema katika shughuli za maendeleo yao ili waweze kuondokana na baadhi ya kero zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.

Aidha Mpenda amewakumbusha wakulima kutumia mvua zilizoanza kunyesha msimu wa mwaka huu katika maeneo mbalimbali, wajikite zaidi katika shughuli za kilimo badala ya kutumia muda wao mwingi kukaa vijiweni na kuzungumzia mambo yanayoweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.

Mpenda alitoa kauli hiyo juzi kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo  vijijini ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika vijiji mbalimbali.


Alisema kuwa licha ya Serikali kuamua kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, hata hivyo bado wananchi wanaowajibu mkubwa  kushiriki kikamilifu badala ya kuiachia peke yake ifanye kila jambo hata lile ambalo halihitaji gharama kubwa.

“Ni lazima sasa wananchi nao wabadilike kwa kushiriki kikamilifu katika kazi za kujitolea ikiwemo ujenzi wa zahanati na mabweni katika maeneo yao, haiwezekani hata kidogo Serikali ndiyo ifanye kila  kitu hata yale yanayohitaji kufanywa na nguvu za wananchi”, alisema Mpenda.

Alifafanua kuwa Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Madaba imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, maji na ujenzi wa barabara kwa lengo la kuboresha na kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.

Vilevile aliongeza kuwa endapo wananchi  hawatakuwa tayari kuunga mkono juhudi hizo, Serikali haitaweza  kutekeleza miradi hiyo kwa wakati mmoja kutokana na ufinyu wa fedha.

Alisema licha ya fedha kuwa kidogo inayopangwa katika bajeti kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani na zile zinazoletwa na Serikali kuu, halmashauri hiyo imejipanga kuhakikisha kila mradi unakamilika kwa wakati ili kuleta tija kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mpenda amewataka watumishi wa halmashauri ya Madaba kufanya kazi kwa kujituma wakati wote  jambo ambalo ana imani kwamba likizingatiwa litasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

No comments: