Sunday, December 31, 2017

MADABA WALIA NA SOKO LA TANGAWIZI WAIOMBA SERIKALI IWASAIDIE WAKULIMA


Baadhi ya wakulima wa Tangawizi katika kijiji cha Magingo Halmashauri ya Madaba wakiandaa tangawizi kabla ya kuziweka ndani ya magunia na kusafirisha kwenda sokoni, hata hivyo zao hilo limekumbwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika jambo linalowafanya wakulima hao kuuza zao hilo kwa bei ndogo.


Na Muhidin Amri,    
Madaba.

BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao la tangawizi katika kijiji cha Magingo na Mkongotema, kata ya Mkongotema Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuwatafutia soko la kuuza zao hilo ili kuweza kukomesha vitendo vya walanguzi wanaokwenda kuwalaghai wakulima hao kununua tangawizi kwa bei ndogo.

Hali hiyo imefuatia kuporomoka kwa bei ya zao hilo katika jimbo la Madaba kutoka shilingi 4,000 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi 700 mwaka 2017 hivyo kuwafanya wakulima hao kuvunjika moyo wa kuendeleza kuzalisha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari waliotembelea wakulima hao ili kujionea changamoto hiyo walisema kuwa wakati umefika sasa kwa Serikali kutambua matatizo ya wakulima wa zao la tangawizi na kuyatafuta ufumbuzi wa haraka.


Wakulima hao Michael Gumbo na Paul Sanga walisema wanalazimika kuuza kwa bei hiyo ndogo ambayo hailingani na gharama halisi ya uzalishaji na hatimaye huwafanya kupata hasara.

Walifafanua kuwa kwa muda mrefu sasa walanguzi  wa ndani na nje ya mkoa huo kwa nyakati tofauti huwasili mkoani humo hadi mashambani kwa wakulima na kununua tangawizi kwa bei ya chini na kwenda nayo kuuza kwa bei ya juu maeneo mengine jambo ambalo wanaiomba Serikali iingilie kati na kunusuru hali hiyo.

No comments: