Tuesday, December 19, 2017

MABENKI TUNDURU YATAKIWA KUSOGEZA HUDUMA KARIBU NA WANANCHI

Baadhi ya wakulima wa zao la korosho wilayani Tunduru wakiwa katika foleni kwa ajili ya kupata huduma ya kufungua akaunt zao benki kutoka kwa mmoja wa wakala katika mji wa Tunduru, Serikali imeelekeza kila mkulima alipwe fedha zake kupitia benki ili kuzuia uwezekano wa kuibiwa fedha wanazolipwa.


Na Muhidin Amri,     
Tunduru.

SERIKALI imeyataka mabenki yanayotoa huduma Wilayani Tunduru mkoani hapa, kuandaa utaratibu wa kupeleka huduma hizo vijijini ikiwa ni juhudi ya kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mchoteka wilayani humo waliojitokeza katika shughuli ya Mnada wa sita wa kuuza zao la korosho uliofanyika katika Chama cha ushirika cha wakulima Litunguru Amcos.

Homera alilazimika kutoa ushauri huo, baada ya kubaini uwepo wa uhitaji wa huduma hiyo kwa wananchi hasa wakati huu wa mauzo ya zao hilo.


Alisema endapo mabenki hayo yatashindwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati watafute mawakala watakao weza kuwakilisha utendaji kazi wa benki hizo katika maeneo hayo ili kuwaondolea adha wakulima wa korosho ambao hivi sasa wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo Tunduru mjini.

Awali akitoa maelekezo ya mnada huo Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) tawi la Tunduru, Jafari Matata alisema minada hiyo hufanyika baada ya chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru (TAMCU) kusambaza vijarida vinavyoonesha ubora na idadi ya kiasi cha kilo za korosho zitakazouzwa katika mnada husika kwa wanunuzi wote.

Matata alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa taratibu hizo za kisheria wanunuzi huandika barua za kuomba kununua Korosho hizo wakiwa wameainisha bei na kiasi wanachokihitaji, ambapo wakati wa mnada husika barua hizo husomwa mbele ya wakulima na kutoa nafasi kwao kuchagua bei iliyowaridhisha na kuridhia kuuza korosho zao.

Baada ya kutolewa kwa maelekezo hayo wakulima hao huridhia kuuza korosho zao kwa bei ya wastani wa shilingi 3,771.49 kwa kila kilo moja ya korosho ambayo ilikuwa imeingizwa katika maghala ya kuuzia.

Akitoa taarifa za mauzo ya mnada huo naye Meneja wa chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru (TAMCU) Imani Kalembo alisema kuwa katika mnada huo jumla ja tani 2,538 zilipangwa kuuzwa katika mnada huo.

Hata hivyo baada ya wakulima kuridhia kuuza kiasi hicho cha tani 2,538 chama hicho kimefikisha jumla ya mauzo ya tani 16,281.683 za korosho zilizokusanywa kutoka kwa wakulima wilayani humo katika msimu huu wa mwaka 2017/2018.

No comments: